Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa amemtaka Wakala wa Majengo hapa nchini (TBA), kuhakikisha anakamilisha kwa wakati ujenzi wa miradi mbalimbali anayotekeleza 
Waziri Mbarawa ameyasema hayo wakati akikagua Ujenzi wa Hospitali ya Mkoa, Nyumba za Viongozi wa Mkoa zinazojengwa na Wakala huyo eneo la Nyaumata mjini Bariadi wakati wa ziara yake Mkoani Simiyu.
Amesema kuwa TBA ni Taasisi ya Serikali ambayo imeaminiwa na Serikali kwa kuwa inafanya kazi vizuri lakini imekuwa ikichelewa kukamilisha miradi inayopewa tofauti na muda uliowekwa kulingana na mikataba.
“TBA ni Taasisi ya Serikali na katika Serikali hii ya awamu ya tano tumeipa miradi mingi tukiamini kuwa watafanya kazi nzuri zenye ubora na kukamilika kwa wakati, ubora upo lakini tatizo kubwa ni kutomaliza kazi kwa wakati” alisema Waziri Mbarawa.
“TBA mjipange mhakikishe mnamaliza miradi kwa wakati vinginevyo hatutawapa kazi kwa sababu hatuwezi kuwapa fedha za Serikali jengo la mwaka mmoja mnajenga miaka mitano, naamini mkijipanga vizuri uwezo mnao na Serikali inawaamini” alisema Mbarawa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka pia ametoa wito kwa Wakala wa majengo TBA kukamilisha ujenzi wa Nyumba za Viongozi wa Mkoa huo ili viongozi waweze kupata makazi .
Wakati huo huo Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Ndg.Jumanne Sagini amesema kuwa ameshalipa fedha kwa TBA ili waweze kukamilisha ujenzi wa Nyumba za Viongozi wa Mkoa na wameahidi kukamilisha na kukabidhi nyumba hizo mwezi Mei mwaka huu.
Awali akitoa maelezo ya Miradi inayotekelezwa na TBA mkoani Simiyu, Meneja wa TBA mkoani humo Mhandisi.Likimaitare Naunga amesema wanashindwa kukamilisha baadhi ya miradi kwa wakati kutokana na kucheleweshewa fedha.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment