Agizo hilo amelitoa wilayani Meatu, mara baada ya kukagua miradi ya maji ya Lubiga, Itinje na Bukundi na kutoridhishwa na kazi iliyofanyika.
“Tunasitisha malipo yote ya wakandarasi watatu wanatekeleza miradi saba ya maji ndani ya Wilaya ya Meatu, malipo yafanyike baada ya Wataalam wetu wanasheria, wahandisi wa maji wa Halmashauri ya Meatu, Mhandisi wa Maji Mkoa, Mwanasheria ya Mkoa na timu ya Mkoa kujiridhisha; ikiwa wanastahili kulipwa watalipwa ikibainika hawana sifa tunavunja mkataba” alisisitiza Mtaka.
Pamoja na kusitisha malipo hayo Mtaka amesema makampuni hayo hayataruhusiwa kufanya kazi za ukandarasi katika miradi yoyote wilayani humo.
Katika hatua nyingine Mtaka amewataka Viongozi wa Kisiasa wilayani Meatu wanaomiliki Makampuni ya Ukandarasi kuacha mara moja kuomba kazi za ujenzi wa miradi mbalimbali katika Halmashauri hiyo badala yake waombe katika Halmashauri jirani Mkoani humo ili kuepuka mgongano wa kimaslahi.
Aidha, amekemea tabia ya baadhi ya viongozi hao wa kisiasa ya kuwapigia simu watumishi wa Halmashauri kwa lengo la kuomba kazi au kudai malipo ya kazi zao na akawahadharisha kuwa endapo hawataacha tabia hii majina yao yatawekwa wazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Ndg.Fabian Manoza amesema kuwa wakandarasi hao waliochaguliwa na bodi ya zabuni na kupitishwa katika vikao vya baraza la madiwani kutekeleza miradi hiyo hawana uwezo.
“Wakandarasi wanaotekeleza miradi hii hawana uwezo wanasubiri walipwe ndiyo kazi ifanyike, pia nikiri kuwa ni kweli kabisa miradi hii inatekelezwa na wanasiasa ndiyo maana hii Halmashauri ya Meatu kuiongoza tunapata shida sana, pale unaposimamia sheria unaitwa kwenye vikao na kuazimiwa, lakini kama viongozi hasa tulioteuliwa tutasimamia sheria na taratibu” alisema Manoza.
Naye Afisa Ugavi ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Manunuzi Ndg. Emmanuel Marwa amesema kuwa taratibu za manunuzi hazikufuatwa katika upatikanaji wa wakandarasi hao ikiwa ni pamoja na Kampuni moja kupewa kusaini mkataba wa kazi zaidi ya moja.
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe.Dkt.Joseph Chilongani, ameunga mkono agizo la Mkuu wa Mkoa la kusitisha malipo na kuangalia namna ya kuvunja mikataba na akabainisha kuwa wamekuwa wakikumbana na changamoto katika utekelezaji wa sheria na maelekezo mbalimbali kutokana na baadhi ya viongozi kuingilia utekelezaji hivyo ni vema hatua zichukuliwe.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment