Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani
akizungumza wakati wa Mkutano wake na Jumuiya ya Wamiliki wa Viwanda
uliofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Kaimu Kamishna wa
Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga na Mwenyekiti wa
Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Salum Shamte.
Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati
Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga akizungumza jambo wakati wa Mkutano wa
Waziri wa Nishati na Jumuiya ya Wamiliki wa Viwanda uliofanyika jijini
Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi
(TPSF), Salum Shamte akizungumza wakati wa Mkutano wa Waziri wa Nishati
na Jumuiya ya Wamiliki wa Viwanda uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Kushoto kwake ni Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi
Innocent Luoga.
Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi,
Mwanamani Kidaya (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya
Utawala, Wizara ya Nishati, Zahara Guga wakifuatilia masuala mbalimbali
yaliyokuwa yakijadiliwa wakati wa Mkutano wa Waziri wa Nishati na
Jumuiya ya Wamiliki wa Viwanda uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Wadau mbalimbali waliohudhuria Mkutano wa Waziri wa Nishati na Jumuiya ya Wamiliki wa Viwanda uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani
(wa pili kushoto), Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua
(wa kwanza kulia), Mwenyekiti wa TPSF, Salum Shamte (wa kwanza kushoto)
na Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye (wa pili kutoka kulia)
wakiwa katika Mkutano na wenye viwanda uliofanyika jijini Dar es Salaam.
…………………………………
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani,
ametoa Siku Saba kwa Mameneja wa TANESCO kote nchini kutembelea viwanda
kwenye maeneo yao kwa lengo la kuhakikisha kuwa viwanda hivyo vinapata
umeme wa uhakika kwa ajili ya uzalishaji na kufanya utatuzi endapo
kutakuwa na changamoto ya kutokuwepo kwa umeme kwenye maeneo hayo.
Aliyasema hayo tarehe 18 Juni, 2019
wakati wa Mkutano wake na Jumuiya ya Wamiliki wa Viwanda ambapo kikao
hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi
Mwinyimvua, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Salum Shamte,
Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, Kaimu Kamishna wa Umeme
na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Kaimu Kamishna wa Petroli
na Gesi, Mwanamani Kidaya, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito
Mwinuka na watendaji wengine kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara na
Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI).
“Nimetoa Siku Saba za kutekeleza suala
hili, na kama hawajatembelea maeneo yenu, wenye Viwanda toeni taarifa
ili tuweze kuchukua hatua lakini na ninyi wamiliki wa viwanda,
hakikisheni kuwa mnalipa bili za umeme la sivyo tutakata umeme.” alisema
Dkt Kalemani.
Kuhusu gharama za umeme aliagiza kuwa,
TANESCO waendelee kutoa gharama halisi za kumuunganishia mteja umeme na
si kulimbikizia gharama hizo hali itakayochelewesha lengo la uanzishaji
wa viwanda vingi nchini.
“Mkifanya makadirio ya gharama za umeme
anazopaswa kulipia mteja hakikisheni kuwa mnaweka gharama halisi kwa
sababu ikitokea umeagizwa kurudia kufanya makadirio hayohayo na
yakashuka, Meneja, utachukuliwa hatua.” alisema Dkt Kalemani.
Kuhusu ushirikishaji wa Sekta binafsi
kwenye Sekta ya Nishati, Dkt Kalemani alisema kuwa, Serikali itaendelea
kushirikiana na Sekta hiyo kwani kukua kwa uchumi wa nchi kunategemea
mashiriakiano kati ya pande hizo mbili.
kuhusu uanzishaji wa viwanda vijijini
alitoa wito kwa wawekezaji hao kuainisha mapema maeneo watakayojenga
viwanda wakati miradi ya umeme vijijini ikiendelea kutekelezwa ili
kusogeza miundombinu ya umeme kwenye maeneo kabla ya viwanda kujengwa.
kwa upande wake, Mwenyekiti wa TPSF,
Salum Shamte, alimpongeza Waziri wa Nishati kwa kuitisha mkutano huo
muhimu na kuweza kutoa maagizo ya papo kwa papo ya kutatua baadhi ya
changamoto zilizoainishwa na wenye viwanda hao pia kwa kuahidi kutatua
changamoto zote zilizoainishwa kwenye Mkutano huo.
Alitoa wito kwa Serikali kuzingatia suala
la kuwapa kipaumbele wazawa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
Nishati na kupongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali
kuboresha hali ya umeme nchini kupitia miradi ya uzalishaji,
usafirishaji na usambazaji umeme.
Kikao cha Waziri wa Nishati na wenye
viwanda kililenga kusikiliza changamoto na maoni ya wenye viwanda hao
kuhusu nishati ya umeme na Gesi na kujadiliana kuhusu utatuzi wake
ambapo wadau hao walipata fursa ya kutoa maoni mbalimbali ambayo Wizara
ya Nishati kupitia Taasisi zake iliahidi kuyafanyia kazi.
0 comments:
Post a Comment