MKUU wa wilaya ya Ikungi mh Miraji Mtaturu
amesherehekea sikukuu ya Eid El Fitri pamoja na wanafunzi wenye mahitaji maalum
na walimu wa shule ya msingi Ikungi.
Viongozi wengine walioshiriki ni pamoja na
viongozi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wilayani humo, masheikh na wachungaji.
Akizungumza mara baada ya kupata chakula na watoto hao, mh Mtaturu, amesema
lengo la kusherehekea na wanafunzi hao ni kuwafanya wajione ni watu muhimu sana
kwa jamii.
Amesema jamii ya wenye mahitaji maalum
wanahitaji kuangaliwa kwa jicho la pekee, ikiwamo kutoa kipaumbele kwa kutatua
changamoto zao nyingi zinazowakabili.
"Watoto wetu hawa wanahitaji upendo wetu,
na sisi kama serikali tutaendelea kuwaenzi na kushirikiana nao pamoja katika
kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili, "alisema mh Mtaturu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya
Ikungi Justice Kijazi amesema wanatoa kipaumbele kwa kundi hilo kwa kuwa
wanatambua umuhimu na mchango wao
katika maendeleo yao binafsi na Taifa
kwa ujumla.
"Katika kutekeleza kwa vitendo
halmashauri imetengeneza mashine nane za kuandikia watoto wenye mahitaji
maalum, ikiwa ni pamoja na kuwapa karatasi maalum za kusomea na kutatua
changamoto kubwa waliyokuwa nayo kwa muda mrefu, "alisema mkurugenzi huyo.
Amesema malengo ya halmashauri ni kuwasaidia
wanafunzi hao ili wasome bila kikwazo na kufikia ndoto zao maishani bila kujali
changamoto za kimaumbile walizonazo.
“Tuko bega kwa bega kuwasaidia watoto wenye
mahitaji maalum ili wasome kama watoto wengine wasio na changamoto za maumbile,
tunatendelea kutenga bajeti kwa ajili ya na kuhakikisha inawafikia kwa kutatua
changamoto zozote zilizopo,” alibainisha.
Wakizungumza mara baada ya chakula hicho,
wanafunzi hao wamepongeza uamuzi wa Mkuu wa wilaya kuandaa chakula hicho kwa
kuwa amewajali na kuonyesha anawapenda.
"Huu upendo ni mkubwa kwetu, kwa kuwa
katika maisha yetu hatukutarajia kuhudumiwa au kula chakula pamoja na viongozi
wa ngazi ya juu ya wilaya hii na ni mara
ya kwanza kufanyika hafla kama
hii,alisema mmoja wa wanafunzi hao.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment