METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, June 5, 2019

DC MTATURU ASHEREHEKEA EID EL FITR NA NA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM


 




MKUU wa wilaya ya Ikungi mh Miraji Mtaturu amesherehekea sikukuu ya Eid El Fitri pamoja na wanafunzi wenye mahitaji maalum na walimu wa shule ya msingi Ikungi.

Viongozi wengine walioshiriki ni pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wilayani humo, masheikh na wachungaji.

Akizungumza mara baada ya kupata  chakula na watoto hao, mh Mtaturu, amesema lengo la kusherehekea na wanafunzi hao ni kuwafanya wajione ni watu muhimu sana kwa jamii.

Amesema jamii ya wenye mahitaji maalum wanahitaji kuangaliwa kwa jicho la pekee, ikiwamo kutoa kipaumbele kwa kutatua changamoto zao nyingi zinazowakabili.

"Watoto wetu hawa wanahitaji upendo wetu, na sisi kama serikali tutaendelea kuwaenzi na kushirikiana nao pamoja katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili, "alisema mh Mtaturu.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ikungi Justice Kijazi amesema wanatoa kipaumbele kwa kundi hilo kwa kuwa wanatambua umuhimu  na mchango wao katika  maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.

"Katika kutekeleza kwa vitendo halmashauri imetengeneza mashine nane za kuandikia watoto wenye mahitaji maalum, ikiwa ni pamoja na kuwapa karatasi maalum za kusomea na kutatua changamoto kubwa waliyokuwa nayo kwa muda mrefu, "alisema mkurugenzi huyo.

Amesema malengo ya halmashauri ni kuwasaidia wanafunzi hao ili wasome bila kikwazo na kufikia ndoto zao maishani bila kujali changamoto za kimaumbile walizonazo.

“Tuko bega kwa bega kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum ili wasome kama watoto wengine wasio na changamoto za maumbile, tunatendelea kutenga bajeti kwa ajili ya na kuhakikisha inawafikia kwa kutatua changamoto zozote zilizopo,” alibainisha.

Wakizungumza mara baada ya chakula hicho, wanafunzi hao wamepongeza uamuzi wa Mkuu wa wilaya kuandaa chakula hicho kwa kuwa amewajali na kuonyesha anawapenda.

"Huu upendo ni mkubwa kwetu, kwa kuwa katika maisha yetu hatukutarajia kuhudumiwa au kula chakula pamoja na viongozi wa ngazi ya juu ya wilaya hii na  ni mara ya kwanza kufanyika  hafla kama hii,alisema mmoja wa wanafunzi hao.

Mwisho.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com