MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa Thuwayba
Edington Kisasi akifungua mafunzo ya kuhamasisha daftari la wapiga kura
na suala la mikopo kwa wanawake viongozi wa UWT mkoa mkoa wa Kaskazini
Unguja. Kulia ni Mbunge wa viti maalumu wa mkoa huo, Angelina Adam
Malembeka kushoto ni Mwenyekiti wa UWT Mkoani humo Maryam Muharami
Shomari.
MBUNGE wa viti maalumu mkoa wa Kaskazini
Unguja, Angelina Adam Malembeka (kulia) akihamasisha jambo kwenye
mkutano mafunzo ya kuhamasisha daftari la wapiga kura na suala la mikopo
kwa wanawake viongozi wa UWT mkoa mkoa wa Kaskazini Unguja.
MGENI rasmi katika mkutano huo, Thuwayba
Edington Kisasi (wa tatu kulia) katika picha ya pamoja na viongozi wa
UWT mkoa wa Kaskazini Unguja, watatu kushoto ni Mbunge wa viti maalun
nkoani humo Angelina Adam Malembeka
MBUNGE wa viti maalumu mkoa wa Kaskazini
Unguja, Angelina Adam Malembeka (kushoto) akihamasisha wanawake viongozi
wa UWT wa mkoa wa Kaskazini Unguja juu ya daftari la wapiga kura na
sala la mikopo kwa wanawake wa UWT kwenye kumbi wa mikutano wa CCM mkoa.
(PICHA NA MARTIN KABEMBA).
………………
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR
VIONGOZI na wanachama wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kaskazini Unguja wametakiwa kuwasaidia viongozi
waliochaguliwa kuteleleza ilani na ahadi walizozitoa wakati wa uchaguzi
uliopita badala ya kukumbatia wagombea wa uchaguzi ujao.
Akifungua mafunzo ya siku moja
yaliyoshirikisha viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa CCM
mkoani humo, Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa Thuwayba Eddington Kisasi
alieleza kuwa kufanya hivyo kunapelekea viongozi waliopo madarakani
kushindwa kusimamia ahadi zao.
Alisema wapo baadhi ya viongozi wa chama
lkatika ngazi mbali mbali wameanza kuwakumbatia wanachama
‘wanaojipitishapitisha’ kwa lengo la kuwania nafasi za uongozi katika
uchaguzi mkuu ujao watambue kuwa kufanya hivyo wakati huu ni kukiuka
kanuni za uchaguzi za chama hicho.
Mafunzo hayo yaliyolenga kuhamasisha
ujasiriamali na mikopo kwa wanawake na uimarishaji wa daftari la kudumu
la wapiga kura yaliandaliwa kwa pamoja kati ya mbunge wa viti maalum
Mkoa wa Kaskazini Unguja Angelina Adam Malembeka na UWT Mkoa ikiwa ni
sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi iliyoagiza kuinuliwa kwa hali
za kiuchumi za wanawake katika ngazi zote.
Alisema kanuni za uchaguzi za CCM
zinakataza mtu kufanya kampeni kabla ya wakati hivyo viongozi wanaoandaa
wagombea na kupanga nao mikakati wanapaswa kujua kuwa wanachochea
vurugu ambazo zinakwaza kasi ya utekelezaji wa ilani na kuchelewesha
upatikanaji wa maendeleo ya jamii.
“Chama kiliweka muongozo na ndio maana
Mwenyekiti wetu (Dk. John Magufuli) alikataza Mambo ya mikutano ya
hadhara ya vyama vya siasa ili tupate kuteleleza ahadi tulizoweka kwa
wananchi wetu na nyinyi no mashahidi kwamba kabla ya 2020
tumeshatekeleza ilani kwa zaidi ya asilimia 90 Tanzania bara na
Zanzibar”, alieleza Kisasi.
Aidha aliwataka viongozi hao kuwa
mabalozi wazuri na kuisambaza elimu waliyopatiwa kwa wanachama wenzao
kwani yana umuhimu mkubwa katika maendeleo ya jamii na siasa za
Tanzania.
“Tuliahidi kuinua uchumi wa wanawake
katika ilani ya uchaguzi kupitia njia mbali mbali zikiwemo za
ujasiriamali na uanzishwaji wa viwanda hivyo mafunzo haya yana mchango
mkubwa katika kuendeleza vikundi vya kiuchumi tulivyonavyo katika
shehia, wadi, wilaya na mikoa yetu”, alisema Makamu huyo wa Mwenyekiti.
Aidha aliwataka wajasiriamali nchini
kutumia fursa ya marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki iliyoanza
Juni mosi mwaka huu Tanzania bara, kutengeneza mifuko mbadala ya kubebea
bidhaa na kuipeleka huko ili kujiendeleza kiuchumi.
Akizungumzia uimarishaji wa daftari la
kudumu la wapiga kura, Kisasi aliwataka wanawake kuwa mstari wa mbele
kuhamasisha jamii kwenda kuhakikisha taarifa zao na kuwasaidia vijana
wenye sifa waweze kujiandikisha.
“Utekelezaji wa ibara ya 5 ya katiba ya
chama chetu wa kushinda uchaguzi haupo wakati wa uchaguzi pekee bali
huanza mapema na huu ndio wakati wake ili kuzichungachunga kura za
ushindi wetu ifikapo 2020”, alieleza Makamu Mwenyekiti huyo.
Akiwasilisha mada juu ya ujasiriamali na
mikopo Mkurugenzi wa taasisi inayojihusisha na elimu ya ujasiriamali na
utoaji wa mikopo ya jijini Dar es salam Nickson Martin alisema ili kuwa
na uzalishaji wenye tija ipo haja ya wajasiriamali kuzingatia elimu na
uwekaji kumbukumbu za biashara zao kujua maendeleo ya shughuli zao.
“Ni lazima mkubali kubadilika na kuweka
mikakati kuzifikisha ndoto zenu na za serikali yetu ya kuimarisha uchumi
wa watu wake kupitia uchumi wa viwanda”, alisema Nickson.
Nae Katibu Msaidizi wa CCM mkoani humo
Shafi Hamad Ali akiwasilisha mada ya umuhimu wa daftari la kudumu
alisema viongozi wa ngazi zote za chama hicho wanapaswa kujidhatiti na
kuhakikisha wanatekeleza maagizo na maelekezo ya chama kama
inavyoelekezwa na katiba ya CCM na ya jumuiya zake.
“Msingi wa ushindi katika uchaguzi wa
chama chetu ni umoja na mshikamano na ndio maana sote tunawajibika
kuhakikisha chama kinashinda katika chaguzi za kutafuta dola na daftari
ndio chanzo cha ushindi siku zote”, alisema Shafi.
Akitoa shukran za washiriki wa mafunzo
hayo Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja Angelina Adam
Malembeka alieleza kuwa ataendelea kuwatafutia wanawake wa mkoa huo
fursa za kujikomboa kiuchumi ili waweze kujitegemea na kusaidia
maendeleo ya familia zao.
Alisema iwapo wanawake hao watatumia
kikamilifu fursa za mikopo inayotolewa na taasisi za serikali na za
binafsi wanaweza kupiga hatua kubwa za maendeleo ikiwa ni pamoja na
kuanzisha viwanda.
Alisema mafunzo hayo ni mwendelezo wa
mafunzo aliyowahi kuwapatia wananchi wa mkoa huo kwsa kushirikiana na
wadau mbali mbali ambapo hapo awali makundi mbali mbali ya wanawake
yalipatiwa mafunzo ya utengenezaji chaki na mishumaa ili kujiongezea
kipato.
“Baada ya kupata mafunzo yale nimeona
nije na haya ya kuwaonesha fursa za kuendeleza miradi yetu ili siku moja
tuwe na viwanda vidogo vidogo na vya Kati, hapo tutakuwa tumejikomboa
kiuchumi kweli kweli”, alisema Malembeka.
Alizungumzia mafunzo hayo mmoja ya
washiriki wa mafunzo hayo ambae ni Katibu wa UWT jimbo la Kijini Maryam
Rashid Mussa alisema yamewasidia kuziona na kutambua fursa za misaada na
kwamba watayatumia kuimarisha mitaji yao na chama kwa ujumla.
Mafunzo hayo yalishirikisha jumla ya
viongozi wajumbe wa mkutano mkuu wa mkoa huo 120 yalifungwa na Mjumbe
wa Halmashauri Kuu ya taifa anaetokea jumuiya ya wazazi Tanzania
Suleiman Juma Kimea ambae aliwasisitiza washiriki mafunzo hayo
kusimamamia misingi na maadili ya chama hicho ili kuepuka mizozo isiyo
ya lazima.
0 comments:
Post a Comment