*********************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameutaka uongozi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) ukamilishe
majadiliano yao na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuhusu matumizi
ya kadi za NHIF kwenye hospitali zao ili Watanzania wengi zaidi waweze
kunufaika.
Ametoa kauli hiyo leo mchana
(Jumapili, Mei 26, 2019) alipokutana na viongozi kadhaa wa taasisi hiyo
pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Ummy Mwalimu, ofisini kwake bungeni jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mchango unaotolewa na taasisi ya AKDN katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya.
“Nilijionea kazi kazi kubwa
inayofanyika pale Hospitali ya Aga Khan Machi, mwaka huu, niliongea na
wagonjwa na kupata maoni yao, lakini kikubwa tu mpunguze gharama na
muimarishe huduma zenu,” amesema.
Amewapongeza viongozi hao kwa
utoaji wao wa huduma kwenye sekta nyingine kama elimu, maji na kilimo.
“Tunategemea mtaendelea kuimarisha huduma hizo ili ziwasaidie Watanzania
wengi zaidi,” amesisitiza.
Viongozi hao walikutana na Waziri
Mkuu ili kumuarifu juu ya mpango wa taasisi hiyo wa kuanzisha kituo
maalum cha matibabu ya saratani nchini (Specialised Cancer Care
Facility) ambao unatarajiwa kugharimu dola za marekani milioni 15. Kituo
hicho kitaendeshwa kwa ubia baina ya hospitali za Ocean Road,
Muhimbili, Bugando na Aga Khan.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu alimweleza
Waziri Mkuu kwamba hospitali za Ocean Road na Bugando zinatoa huduma za
radiotherapy na chemotherapy, wakati hospitali ya KCMC inatoa huduma ya chemotherapy tu. “Hospitali ya Rufaa ya Mbeya bado huduma hizo zinaadaliwa ili ziweze kutolewa,” alisema.
Hata hivyo, Waziri Ummy alisema
hivi sasa kwa nchi nzima, kuna vituo zaidi ya 120 ambavyo vinatoa huduma
ya utambuzi wa saratani (cancer screening).
Mapema, akitoa maelezo kuhusu
mpango wa kujenga kituo hicho, Mwakilishi Mkazi wa AKDN, Bw. Amin Kurji,
alisema wameshawasiliana na hiospitali zote tajwa na sasa
wanashirikiana na wataalamu wa wizara ya afya ili kukamilisha suala
hilo.
“Tatizo la saratani hapa nchini ni
kubwa kwa sasa. Lakini tunataka watu watambue kwamba ukiugua saratani
haimaanishi kwamba utakufa mara moja (it’s not a death sentence).
Inaweza kutibika endapo mgonjwa atawahi kupata matibabu,” alisema Bw.
Kurji.
Alisema kwa sasa hivi hapa nchini
hakuna kituo maalum cha matibabu ya saratani nchini lakini kitu cha
pekee kuhusu kituo hicho ni uwepo wa huduma zinazotembea za upimaji na
utoaji tiba hadi mikoani. “Huduma hizi zitakuwa zinatolewa kwenye mikoa
yote kupitia njia ya mtandao, ilhali vituo vikuu vya Dar es Salaam na
Mwanza vitakuwa vikitoa majibu kwa madaktari husika,” alisema.
Alisema lengo lao pia ni kutoa
elimu juu ya kuzuia, upimaji wa mapema na upatikanaji wa tiba
(prevention, early diagnosis and cure).
0 comments:
Post a Comment