Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali
Bungeni jijini Dodoma, Mei 23, 2019.
*Ni baada ya Serikali kusikia kilio kutoka
kwa wafanyabiashara
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali
imeanza jitihada za kufuta tozo zote ambazo zinakwamisha mazingira ya ufanyaji wa
biashara nchini zikiwemo za kwenye pembejeo ili kuwawezesha wafanyabiashara
kuzifikisha hadi ngazi ya kijiji kwa wakulima.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Mei 23,
2019) Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Madaba, Kizito
Mhagama katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kujua
Serikali ina mpango gani wa kupunguza tozo kwa maduka yanayouza pembejeo ili
kumwezesha mkulima kupata pembejeo.
Waziri Mkuu amesema Serikali imepokea
malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo na wauzaji wa
pembejeo juu ya tozo mbalimbali katika uendeshaji wa shughuli nzima wa
biasharazao.
“Serikali imesikia vilio vyenu na sasa
inafanya mapitio ya tozo hizo na itakapofikia hatua nzuri itawajulisha na
kuwashirikisha kujua ni aina gani ya tozo ambayo itaondolewa au kuibadilisha
ili muendelee kufanya biashara zenu katika mazingira rahisi.”
Waziri Mkuu amesema kazi kubwa inayofanywa na
Serikali kwa sasa ni kufanya mapitio ya tozo zote kuanzia kwa wakulima hadi kwa
wafanyabiashara na kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara nchini,
ikiwemo ya pembejeo ili kuzifikisha kiurahisi kwa wakulima.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kwamba tayari
Mawaziri wa kisekta wenye dhamana ambao wana tozo mbalimbali kwenye wizara zao
zinazokwamisha ufanyaji biashara katika mazingira rafiki wameshakutana kwa
ajili ya kujadili namna ya kulipatia ufumbuzi suala hilo.
“Hata juzi nilikuwa na mawaziri hao kupata
taarifa zao kwa pamoja kuona maeneo yote waliyoyapitia na tozo zote
zinazokusudiwa kupitiwa upya na kazi hiyo ikikamilika watakutana na Kamati ya
Bajeti ya Bunge, Wizara ya Fedha ili kuona namna nzuri ya kuondoa tozo hizo.
Lakini baadaye suala hilo litaenda kwenye mamlaka inayotoa ridhaa ya kuondoa au
kupunguza tozo.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema miradi mingi ya maji
ambayo inatekelezwa kwenye maeneo mbalimbali nchini baadhi yake haitekelezwi
kwa viwango vilivyokusudiwa, hivyo haiwiani na thamani halisi ya kiasi cha
fedha kinachotolewa.
Hata hivyo Waziri wa Maji wakati akiwasilisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2019/2020 alieleza
hatua mbalimbali zilizochukuliwa dhidi ya miradi yote ambayo haiwiani na kiasi
cha fedha kilichotolewa pamoja na hatua zilizochukuliwa dhidi ya miradi yote.
“Moja kati ya hatua ambazo amezifanya ni
pamoja na kuunda timu inayopita kukagua miradi yote nchini na kujiridhisha kama
matengenezo yake yanakidhi thamani ya fedha iliyotolewa katika mradi huo na
kama haukidhi hatua kali zinachukuliwa kwa wahusika.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu
swali la mbunge wa Korogwe Mjini Mary Chatanda aliyetaka kujua Serikali kama
ipo tayari kuchunguza na kuchukua hatua kwa watendaji walioshindwa kusimamia
miradi ya maji na kuisababishia hasara pamoja na wananchi kukosa huduma waliyokusudiwa.
0 comments:
Post a Comment