Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa (Mb) akijibu swali
bungeni leo tarehe 31 Mei 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge
la Bajeti Jijini Dodoma. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya
Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Kulia) pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa (Mb) wakifuatilia kipindi cha maswali na majibu bungeni leo tarehe 31 Mei 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Kwa kipindi cha Mwaka 2006 - 2014, Wizara ya Kilimo kwa
kushirikiana na Uongozi wa Mkoa wa Kagera umetoa mafunzo ya kutokomeza
ugonjwa wa mnyauko wa migomba kwa wakulima na maafisa ugani kwenye wilaya zote
zilizoathirika.
Serikali
imekuwa ikiendesha kampeni ya kung’oa migomba yote iliyoathirika, kukata Ua Dume
na kuiteketeza. Halmashauri zote za Wilaya za Mkoa wa Kagera ziliweka sheria
ndogo ndogo za kuwataka wakulima kung’oa na kuchoma au kuzika migomba yote
iliyoathirika. Zoezi hilo lilipunguza ueneaji wa ugonjwa huo kwa asilimia 70.
Naibu
Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 31 Mei
2019 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe Jasson Samson Rweikiza
Mbunge wa Bukoba vijijini aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango gani kuchukua
hatua za makusudi za kupambana na ugonjwa huo na kutokomeza kabisa.
Bashungwa
alisema kuwa Serikali inaendelea kufanya tafiti za kuzalisha miche bora ambayo
haina vimelea vya ugonjwa wa unyanjano kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo
Tanzania (TARI) ikishirikiana na Shirika la Belgium
Technical Cooperation.
Aidha,
hadi sasa miche bora milioni sita (6) imezalishwa na kusambazwa kwa wakulima katika
Mikoa ya Kagera na Kigoma.
Bashunwa
ametoa wito kwa wakulima kote nchini kutumia mbegu bora za migomba aina ya Shia 17, Shia 23, Nshakara, Nyoya,
na Kinohasha zinazozalishwa katika taasisi za utafiti kama Chuo kikuu cha
Kilimo Sokoine, Mikocheni, Uyole, Kibaha, Maruku na Tengeru ili kuongeza tija
katika uzalishaji na kutosafirisha ndizi zilizofungashwa na majani ya migomba
kutoka mashamba yaliyoathirika.
Aliutaja
ugonjwa huo wa Mnyauko wa migomba ambao kitaalamu unaitwa unyanjano wa migomba
kuwa husababishwa na vimelea aina ya bacteria ambao hushambulia aina zote za migomba
na jamii yake.
Ugonjwa
huo husambazwa na ndege, nyuki, binadamu, ngedere na tumbili; miche
iliyoathirika; vifaa vya shambani vilivyotumika kwenye migomba iliyoathirika na
vifungashio vya kusafirishia ndizi.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment