Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akiwasha umeme katika Kijiji cha Dibamba wilayani Mvomero, Mkoa wa Morogoro.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) akikata utepe kuashia uwashaji umeme katika Kijiji cha Sanganjeru wilayani Gairo Mkoa wa Morogoro. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe.
Wataalam kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani) wakati akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Tabuhoteli wilayani Gairo, Mkoa wa Morogoro.
Na Teresia Mhagama
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, ametoa Wiki Moja kwa wasimamizi
wa mradi wa usambazaji umeme vijijini mkoani Morogoro kutoka Wizara ya Nishati,
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na TANESCO kuhakikisha kuwa wanatatua
changamoto ya nguzo za umeme mkoani Morogoro.
Naibu Waziri alitoa agizo hilo, tarehe 23 Mei, 2019 mkoani Morogoro
wakati alipofanya ziara ya kukagua kazi ya usambazaji umeme vijijini wilayani
Mvomero na Gairo na kuwasha umeme katika Kijiji cha Dibamba wilayani Mvomero na
Kijiji cha Sanganjeru wilayani Gairo.
Agizo la Naibu Waziri limekuja baada ya sampuli ya nguzo za mkandarasi
wa umeme mkoani Morogoro kupimwa na wataalam wa TANESCO na kuonekana kuwa
hazina vigezo huku mkandarasi huyo akidai kuwa sehemu ya nguzo zake
zinafaa kwa matumizi ya umeme.
" Hatutaki kuona mivutano kati ya wakandarasi na
wasimamizi wa miradi ya umeme vijijini kwani inachelewesha upelekaji
umeme kwa wananchi hivyo nawaagiza mtatue suala hili kwa kupima nguzo zote na
Wizara ipate taarifa ndani ya Wiki Moja."alisema Naibu Waziri
Kuhusu kasi ya mkandarasi anayesambaza umeme vijijini mkoani Morogoro,
kampuni ya State Grid, alisema kuwa, bado haridhishwi na kasi ya mkandarasi
huyo na kutoa onyo kuwa Serikali itamchukulia hatua endapo hatatekeleza kazi
kwa mujibu wa mkataba.
Aidha alitoa agizo kwa wazalishaji wa vifaa vya umeme, wasambazaji na
wakandarasi wa umeme vijijini kutatua changamoto zao kwa haraka mara
zinapojitokeza ili kutochelewesha miradi ya umeme vijijini.
Akieleza kuhusu hatua zilizofikiwa na Serikali katika kazi ya usambazaji
umeme vijijini, alibainisha kuwa hadi sasa asilimia 57 ya vijiji nchini tayari
vimesambaziwa umeme kati ya Vijiji 12,268 huku kazi hiyo ikiendelea na kwamba
Tanzania ndiyo inayoongoza katika nchi za Afrika Mashariki kwa usambazaji umeme
vijijini.
" Wakati Serikali ya Awamu ya Tano, inaingia madarakani ilikuta
vijiji 8783 havina umeme kati ya Vijiji 12,268, ndio ikaanza
safari ya kufikisha umeme kwenye vijiji hivyo kupitia miradi mbalimbali ikiwemo
huu wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza, mradi wa ujazilizi Awamu ya Pili
mzunguko wa kwanza na miradi mingine," alisema Mgalu
Kuhusu bei ya umeme aliendelea kusisitiza agizo la Serikali kuwa ni elfu
27,000 tu, awe anasambaza mkandarasi wa umeme vijijini au TANESCO ili kuleta
usawa wa utoaji huduma kwa wananchi.
0 comments:
Post a Comment