Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma
Katika kipindi cha Mwaka wa Fedha
2018/19, zaidi ya shilingi Bilioni 93.8 zimetumika katika uboreshaji wa
miundombinu ya shule 588 ambapo shule 303 ni za msingi na sekondari
285.
Hayo yameelezwa leo, Jijini
Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Bumbwini, Muhammed Amour Muhammed
juu ya juhudi zipi za makusudi ambazo Serikali inakusudia kuchukua ili
kupandisha hali ya ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha Nne.
“Serikali imeendelea kuchukua
hatua mbalimbali ili kuongeza ufaulu katika ngazi mbalimbali za Elimu.
Hatua hizo ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia
kwa kujenga na kufanya ukarabati mkubwa wa miundombinu katika shule
mbalimbali za Serikali nchini,” amesema Ole Nasha.
Ole Nasha amesema kuwa uboreshaji
wa miundombinu uliofanyika katika shule hizo 588 umehusisha madarasa
1,190, mabweni 222, vyoo 2,141, mabwalo 76 na nyumba 99.
Ameongeza kuwa, Serikali
imeendelea kusambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia vikiwemo, vifaa
vya maabara katika shule, na vifaa vya kielimu kwa ajili ya wanafunzi
wenye mahitaji maalum.
Aidha Naibu Waziri Ole Nasha
ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka 2017 hadi Aprili 2019 Serikali
imeajiri jumla ya walimu 17,884 ili kukabiliana na uhaba wa walimu
nchini.
Vile vile Serikali imeendelea
kuimarisha Idara ya Uthibiti Ubora wa Shule kwa kununua na kusambaza
magari 45 ya Uthibiti Ubora wa Shule na Pikipiki 2,897 kwa ajili ya
Maafisa Elimu kata na kuongeza kuwa katika Mwaka wa Fedha 2019/2020
Serikali inatarajia kujenga ofisi 100 za wathibiti ubora wa shule na
kuongeza idadi ya watumishi.
Aidha amesema ufaulu wa wanafunzi
katika mtihani wa kidato cha IV umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka
ambapo katika mwaka 2018 watahiniwa waliofaulu ni asilimia 78.36
ikilinganishwa na asilimia 77.09 ya mwaka 2017, asilimia 70.35 ya mwaka
2016 na asilimia 67.91 ya mwaka 2015.
0 comments:
Post a Comment