Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga (hawapo pichani) kwenye mkutano wa hadhara uliolenga kutatua mgogoro kati yao na mwekezaji ambaye ni kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited tarehe 03 Aprili, 2019.
Kutoka kushoto mbele, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Jasinta Mboneko na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo wakinukuu kero mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga (hawapo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.
Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.
Na Greyson Mwase, Shinyanga
Naibu
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewataka wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo
kilichopo Wilayani Shinyanga Vijijini Mkoani Shinyanga kumpisha mwekezaji ambaye ni mgodi wa uchimbaji wa kati wa madini ya
dhahabu wa kampuni ya Hanan Afro Asia
Geo Engineering (T) Limited kutoka China kuendelea na maandalizi ya uchimbaji wa madini
ya dhahabu, kwa kuwa ndiye aliyewekeza katika kijiji husika kwa kufuata sheria
na kanuni zake.
Naibu
Waziri Nyongo ametoa agizo hilo mapema leo tarehe 03 Aprili, 2019 katika
mkutano wake wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho ikiwa ni sehemu ya ziara
yake katika mkoa wa Shinyanga yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji na
uchenjuaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Katika
ziara yake Naibu Waziri Nyongo aliambatana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,
Jasinta Mboneko, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, Hamis Kamando,
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hoja Mahiba, Mbunge wa Jimbo
la Solwa, Ahmed Salum, wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa,
wataalam kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini pamoja na waandishi wa habari.
Alisema
kuwa, kumekuwepo na mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo
na mwekezaji kutoka nchini China ambaye ni
kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited ambapo malalamiko
yaliwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe
Magufuli katika ziara yake aliyoifanya Wilayani Kahama Machi 10, 2018 ambapo
alielezwa kuhusu unyanyasaji uliofanywa
wakati wa zoezi la uthamini na ulipaji wa fidia kwenye maeneo hayo kwa ajili ya
kupisha uanzishwaji wa mgodi wa uchimbaji wa kati wa madini ya dhahabu.
Aliendelea
kusema kuwa katika kutekeleza agizo la Rais Magufuli Machi 11, 2018 aliyekuwa
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko alitembelea eneo la Mwakitolyo
linalolalamikiwa kwa lengo la kufanya mkutano na kusikiliza malalamiko ya
wananchi ambapo baada ya kusikiliza malalamiko hayo aliahidi kwenda kufanyia
kazi malalamiko yao na kuwapa mrejesho.
Aliendelea
kueleza kuwa, iliundwa timu maalum kwa ajili ya kufanya uchunguzi kulingana na
hadidu rejea iliyokuwa imepewa ambayo iliitaka timu kukutana na viongozi
kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya, kuainisha majina ya wananchi waliolipwa na
ambao hawajalipwa fidia, vigezo vilivyotumika wakati wa uthaminishaji na
ulipaji wa fidia pamoja na mapendekezo mbalimbali.
Nyongo
aliendelea kufafanua kuwa, mara baada ya timu kumaliza kazi yake, ilibainika
kuwa mwekezaji alilipa kiasi cha shilingi bilioni 1.63 kama fidia kwa wananchi waliokuwa katika eneo
husika hivyo zoezi kukamilika kwa asilimia 99.6.
Alisisitiza
kuwa pamoja na wananchi takribani 375 kulipwa fidia bado ilionekana kuwa wananchi
wengi waliolipwa fidia sio wanakijiji wa Mwakitolyo na kuongeza kuwa wananchi
40 tu ndio walioonekana wamiliki halali wa mashamba pamoja na makazi.
Katika
hatua nyingine Naibu Waziri Nyongo aliitaka Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya
Shinyanga kuharakisha upatikanaji wa maeneo mapya kwa ajili ya wanananchi 40
ambao ni wamiliki halali wa makazi na mashamba katika kijiji cha Mwakitolyo ili
mwekezaji aweze kuanza shughuli za uchimbaji mara moja.
Aidha,
Naibu Waziri Nyongo alimtaka Mkurugenzi wa Kampuni ya Henan Afro-Asia Geo
Engineering Co. Limited kuhakikisha anadumisha mahusiano na wananchi wa kijiji
cha Mwakitolyo na kumtaka kuhakikisha anashiriki katika uboreshaji wa huduma za
jamii kama vile afya, elimu, barabara kama Sheria ya Madini pamoja na kanuni
zake inavyofafanua.
Wakati
huo huo Nyongo aliwataka wananchi kumpa ushirikiano mwekezaji ili kufaidi
matunda ya uwekezaji kwenye kijiji chao
ikiwa ni pamoja na ajira kwa wazawa, utoaji wa huduma za vyakula, biashara,
huduma za jamii hivyo kupaisha uchumi wa kijiji hicho.
Aliendelea
kusema kuwa, madini ni mali ya watanzania wote, hivyo baada ya uwekezaji kuanza
kampuni hiyo italipa kodi mbalimbali kwenye halmashauri na Serikali kuu hivyo
kuboresha sekta nyingine kama vile miundombinu, afya, elimu n.k.
Naye
Mbunge wa Solwa, Ahmed Salum akizungumza katika mkutano huo mbali na kumpongeza
Naibu Waziri Nyongo kwa kutatua mgogoro huo, aliwataka wananchi kufanya kazi
kwa bidii huku wakilinda amani ya nchi.
Naye Mkurugenzi
wa Kampuni ya Henan Afro-Asia Geo Engineering Co. Limited, Zhang Jiangho mbali
na kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kutatua mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu, aliahidi
kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Mwakitolyo kwa kuboresha huduma za jamii na kulipa kodi na tozo
mbalimbali za Serikali.
0 comments:
Post a Comment