METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, April 1, 2019

MHE MGUMBA AKUTANA NA VIONGOZI WA TAASISI YA GRANOT GROUP INAYOTOA NAFASI 100 ZA WANAFUNZI WA TANZANIA KUSOMA NCHINI ISRAEL

Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya Granot Group kutoka nchini Israel Bw Yaron Tamir akimkabidhi Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) taarifa kuhusu kazi wanazozifanya katika nchi mbalimbali duniani, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akifanya mazungumzo na viongozi wa taasisi ya Granot Group kutoka nchini Israel iliyoongozwa na Bw Yaron Tamir katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Na Mathias Canal, Dar es salaam

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba (Mb) jana tarehe 31 Machi 2019 alikutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa Taasisi ya Granot Group kutoka nchini Israel wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Bw Yaron Tamir.

Dhifa hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambapo kwa kauli moja wamejadili fursa kwa watanzania kuhusu nafasi za masomo kwa vitendo kwa wanafunzi waliopo katika vyuo vya kilimo duniani kwa kutumia Mfumo wa kubadilishana wanafunzi (internship exchange program) kwenda nchini Israel kujifunza zaidi.

Kwa Tanzania, progamu hiyo ilianza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2015/16 kwa wanafunzi 20 kutoka Chuo cha SUA kwenda nchini Israel, mwaka 2016/17 wanafunzi 30 kutoka vyuo vya SUA, Ukiriguru na Uyole, mwaka 2017/18 wanafunzi 30 kutoka vyuo vya SUA, Ukiriguru, Uyole, Tumbi na Tengeru.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na Mratibu wa Programu hiyo nchini Tanzania, Dkt. Anna Temu ambae ni mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya SUGECO na baadhi ya maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba ameishukuru Taasisi hiyo kwa msaada wanaoutoa kwa wanafunzi wa kitanzania waliopo katika vyuo mbalimbali vya kilimo nchini.

Pia, alisema kuwa, kupitia programu hiyo, idadi ya wataalamu wa masuala ya kilimo nchini itaongezeka kwa sababu wahitimu wa masomo hayo wakirudi Tanzania ni lazima ‘wasambaze’ uzoefu na utaalamu walioupata nchini Israel kwa manufaa yao, wakulima na Taifa kwa ujumla.

Alisema kuwa program hiyo ina umuhimu mkubwa kwa wananfunzi kutoka nchini Tanzania ili kuhakikisha kilimo kinakuwa chenye tija na chenye manufaa kwa mkulima hivyo kuongeza kipato cha mkulima, kutengeneza ajira na pia kuchangia pato la Taifa kwa ujumla.

“Mahusiano baina ya Tanzania na Israel yamezidi kuimalika kwa manufaa ya nchi hizi mbili na pia, wanafunzi wenye sifa stahiki watapatikana kupitia uhakiki wa kina utakaofanyika katika vyuo vyao ili watakaofaulu usaili waweze kwenda nchini Israel kujifunza kwa vitendo zaidi kwa manufaa yao binafsi, vyuo vyao na Taifa kwa ujumla” Alikaririwa Mhe Mgumba wakati akifunga Kikao hicho.


Naye, Mkurugenzi wa taasisi hiyo ya Granot Group kutoka nchini Israel Bw Yaron Tamir alisema kuwa, Taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi ya kutoa mafunzo kwa wanafunzi waliopo vyuoni kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15 hadi sasa ambapo katika Bara la Afrika programu hiyo inatekelezwa katika nchi mbalimbali kama vile Ghana, Togo, Burkina Faso, Benin, Rwanda, Uganda, Ivory Coast n.k.

Tamir alimuhakikishia Naibu Waziri kuwa wanafunzi hao wakifika nchini Israel wanapewa mafunzo ya nadharia darasani baada ya hapo wanapelekwa mashambani kujifunza kwa vitendo kwa muda wa siku tano kwa kila wiki na watakuwa huko kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mkurugenzi huyo aliongezea kusema kuwa, kilimo ni biashara, hivyo, wanafunzi wakiwa Israel watajifunza namna ya kulima kwa tija kwa kuzingatia mbinu bora za kilimo na kutumia zana za kisasa za kilimo na kujua namna ya kupata masoko ya bidhaa watakazozalisha vile vile, wanafunzi hao wataweza kufahamu changamoto zilizopo katika Sekta ya kilimo duniani na njia zinazotumika kuzipunguza.

Dhumuni la safari hiyo ni kuwasaidia vijana waliopo katika vyuo mbalimbali vya kilimo nchini ili waweze kuwa wakulima wakubwa wa mazao mbalimbali kama vile, maparachichi, nyanya na hata ufugaji wa mifugo ya aina mbalimbali kama vile kuku pindi watakapomaliza masomo yao na hivyo kutengeneza ajira kwa vijana wenzao.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Granot Group aliongezea kwa kusema kuwa, mwaka huu, wametoa nafasi 100 kwa vijana waliopo katika vyuo mbalimbali vya kilimo nchini kwenda Israel kujifunza kwa vitendo kwa kipindi cha mwaka mmoja ikiwa ni sehemu ya masomo ya wanafunzi hao vyuoni kwao.

Alisema kuwa, vigezo vinavyohitajika kwa wanafunzi hao kushiriki safari hiyo ni pamoja na: mwombaji kuwa mwanafunzi katika Chuo cha kilimo, awe raia wa Tanzania anaeweza kuongeza kwa ufasaha lugha ya kiingereza, mchapakazi, mwajibikaji na mwenye uwezo wa kuishi na watu wa mataifa mbalimbali duniani.

MWISHO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com