Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) Kanda ya Afrika Prof Shaukat Abdulrazak Ofisini kwake Jijini Dodoma, leo tarehe 13 Machi 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) Kanda ya Afrika Prof Shaukat Abdulrazak akisisitiza jambo wakati akizungumza na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) Jijini Dodoma, leo tarehe 13 Machi 2019.
Wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Kilimo sambamba na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifatilia mazungumzo kati ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) Kanda ya Afrika Prof Shaukat Abdulrazak Ofisini kwake Jijini Dodoma, leo tarehe 13 Machi 2019.
Wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Kilimo sambamba na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifatilia mazungumzo kati ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) Kanda ya Afrika Prof Shaukat Abdulrazak Ofisini kwake Jijini Dodoma, leo tarehe 13 Machi 2019.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Waziri
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 13 Machi 2019 amekutana na kufanya
mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la nguvu za Atomiki Duniani
(IAEA) Kanda ya Afrika Prof Shaukat Abdulrazak.
Katika Mkutano huo uliotuama kwa masaa kadhaa katika Ukumbi wa
Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma Waziri Hasunga amemueleza Prf Shaukat kuwa
serikali ya Tanzania inaendelea na mchakato wa kubaini wafanyabiashara wanaouza
mbegu feki kwa wakulima kwani wanasababisha hasara kwa wananchi na Taifa kwa
ujumla wake.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi Duniani ambazo wananchi wake
wa wamekuwa wakiuziwa mbegu feki jambo ambalo serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Mhe Rais Dkt john Pombe Magufuli imetilia mkazo kadhia hiyo na
watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Kadhalika, Waziri Hasunga alisema kuwa pamoja na Wizara ya Kilimo
kuendelea na mchakato wa kuboresha kilimo kwa kutumia teknolojia mpya lakini
bado inakabiliwa na uuzwaji wa viuatilifu feki jambo ambalo limefifihisha
juhudi za wakulima kwa muda mrefu.
“Wananchi wetu wanajitahidi kulima kwa kiasi kikubwa lakini
kumekuwepo na changamoto kubwa ya Viuatilifu na Mbegu feki jambo hili hatuwezi
kuliacha kamwe hivyo hivi karibuni nimetangaza kiama na wafanyabiashara
wanaosambaza tutakapowabaini tutawachukulia hatua kali sana” Alikaririwa Mhe
Hasunga
Katika hatua nyingine alieleza kuwa wakulima wengi nchini wamekuwa
wakitumia mazao yao kama mbegu badala ya kutumia mbegu mpya jambo hili
linapunguza kwa kiasi kikubwa ufanisi katika uzalishaji wa mazao.
Akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa
la nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) Kanda ya Afrika Prof Shaukat Abdulrazak
alisema kuwa kukutana na waziri wa Kilimo nchini Tanzania kumeimarisha maradufu
ushirikiano ambao umeanzishwa kwa muda mrefu na shirika hilo.
Alisema kuwa mradi wa nguvu za Atomiki Duniani katika Kanda ya
Afrika unahusisha nchi 45 ambapo unajikita katika uhusiano wa ushirikiano
katika mazao mbalimbali yanayozalishwa.
Alisema katika Visiwa vya Zanzibar Shirika hilo limesaidia kutatua
changamoto kwa kuteketeza magonjwa yote yanayoambukizwa na Mbung’o.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment