Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro katika mkoa wa Geita wakati wa kutoa hati za ardhi kwa wananchi wa mji huo kwenye ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. Kulia kwa Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhandisi Ntemi Musafiri na kushoto ni Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Geita Ally Kidwaka.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chato mkoa wa Geita Eliurd Mwaiteleke alipomkabidhi ramani kwa ajili ya zoezi la urasimishaji katika halmashauri hiyo wakati Naibu Waziri akiwa katika ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro mkoani Geita waliopatiwa hati za ardhi wakati Naibu Waziri akiwa katika ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. Wa tatu kushoto aliyekaa ni Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhandisi Ntemi Musafiri na wa tatu Kulia aliyekaa ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Geita Elisha Lupuga
Mkuu wa idara ya Ardhi na Maliasili katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoa wa Geita Deogratias Matiya akimuonesha Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula eneo la uwekezaji la Lubambagwe (Chato Beach) wakati Naibu waziri akiwa katika ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi mkoani Geita, Kulia ni Meneja wa Shirika la Nyumba mkoa wa Kagera Benit Masika.
Na Munir Shemweta, KATORO
Serikali imehimiza halmashauri nchini kupima maeneo ya
vijiji ili kuwamilikisha wananchi ardhi kwa nia ya kuwapatia hati za kimila na
wakati huo kupanga matumizi bora ya ardhi katika maeneo hayo kwa lengo la
kuepuka migogoro ya ardhi na kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa jana tarehe 12 Februari 2019 na Naibu Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa kutoa hati
21 kwa wananchi wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Katoro uliopo wilaya ya Geita mkoa
wa Geita pamoja na kutoa Ramani za Urasimishaji kwenye wilaya za Chato na Geita
wakati wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia
kodi ya ardhi.
Alisema suala la kupima vijiji ni la lazima na
halmashauri zinapaswa kuchukua hatua za kuwapimia wananchi kwa lengo
la kuwawezesha kiuchumi lakini pia kuleta salama ya miliki ya maeneo yao kwa
kuwa kutofanya hivyo kutasababisha kuwepo migogoro ya mipaka pamoja na kiwanja
kimoja kumilikishwa kwa watu wawili (double allocation).
Akigeukia suala la urasimishaji, Dkt Mabula alizitaka halmashauri
za wilaya ya Geita kuhakikisha zinarasimisha maeneo yaliyojengwa kiholela na
kusisistiza kuwa salama ya eneo la mtu haliishii kuwekewa vigingi bali
kinachotakiwa ni mtu kumilikishwa ili aweze kuitumia ardhi hiyo kujiinua
kiuchumi kwa kuwa anaweza kuitumia hati yake kwa ajili ya kukopea fedha benki,
Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi alikabidhi ramani za urasimishaji kwa wakurugenzi wa
halmashauri mbili za wilaya ya Geita pamoja na ile ya Chato kwa nia
ya kuendesha zoezi la urasimishaji katika maeneo ya halmashauri hizo.
Sambamba na hilo Dkt Mabula alishuhudia utiaji
saini makubailiano ya kupatiwa kiasi cha shilingi milioni 180 kwa
halmashauri ya wilaya ya Geita kwa ajili ya kutwaa maeneo mapya ya halmashauri
hiyo ambapo alieleza kiasi hicho cha fedha kitumike kuepuka kero
wakati wa kutwaa maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, fedha zilizosainiwa ni kama mkopo na halmashauri husika
inatakiwa kuuza viwanja na kurejesha fedha hizo ndani ya miezi mitatu na
kubainisha kuwa Wizara imetengewa shilingi bilioni 7 kwa ajili ya
kuzikopesha halmashauri mbalimbali nchini ili kutwaa maeneo.
Alisisitiza kuwa ni marufuku kuchukua eneo la mtu bila kulipa
fidia na kubainisha kuwa sheria ya mwaka 2016 inaweka wazi kuwa ukitwaa eneo
ndani ya miaka miwili kama hujalipa fidia basi mwenye eneo anaruhusiwa kubaki
na eneo lake na kiasi cha riba kinaongezeka kila baada ya miezi sita.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Geita Ally Kidwaka alisema
pamoja na Halmashauri yake kuwa na miji midogo yenye wakazi 50,000 lakini Mji
Mdogo wa Katoro ndiyo unaokuwa kwa kasi na sasa umefikia wakazi wapatao laki
moja. Alisema kutokana na mji huo kukuwa kwa kasi wataalamu wa upimaji
wanatakiwa kuongezwa katika mji huo ili kuepuka changamoto za urasimishaji
maeneo ya mji huo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halamashauri ya Wilaya ya Geita
Elisha Lupuga alisema Mji wa Katoro pamoja na kukuwa kwa kasi kwa muda mrefu
lakini ulichelewa kupatiwa mamlaka ya Mji jambo
lililochelewesha maendeleo katika mji huo. Hata hivyo,
alisema pamoja na wananchi wa Mji wa Katoro kuwa na uwezo wa fedha
na nyumba nzuri lakini wamekuwa wazito kutoa fedha kwa ajili ya kupimiwa maeneo
yao jambo linalosababisha mji kutopangika vizuri.
------------------------------ ------------------MWISHO------ ------------------------------ ----------------
0 comments:
Post a Comment