METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, March 30, 2019

Shirika la AGPAHI latoa mafunzo ya saikolojia kwa watumishi wa afya Mwanza

Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) limetoa mafunzo kwa watoa huduma za afya kutoka Vituo vya Afya mkoani Mwanza, yanayolenga kuwajengea uwezo katika kutoa msaada na huduma za kisaikolojia kwa watoto na vijana wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Mafunzo hayo ya siku tano yalianza jumatatu Machi 25, 2019 hadi Ijumaa Machi 30, 2019 katika ukumbi wa “Isamilo Lodge” Jijini Mwanza ambapo yamewashirikisha wataalam wa afya zaidi ya 60 kutoka Halmashauri mbalimbali mkoani Mwanza ikiwemo Nyamagana, Ilemela, Misungwi, Magu, Ukerewe na Buchosa.

Afisa Miradi, Huduma Unganishi kwa Jamii kutoka shirika la AGPAHI, Cecilia Yona amesema mafunzo hayo yatawasaidia watoa huduma za afya katika vituo vya tiba na matunzo kutambua namna bora ya kuwahudumia wateja wao hususani watoto na vijana.

Amesema mafunzo hayo yatawasaidia pia kuwatambua watoto na vijana wenye changamoto kisaiklojia na namna ya kuwasaidia huku wakizingatia upatikanaji wa huduma bora na rafiki kwa wateja kupitia mbinu mbalimbali ikiwemo michezo.

“Tunatarajia pia wataenda kuanzisha vikundi vya akina mama wanaoishi na maambukizi ya VVU ambao wako kwenye kitengo cha kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ili nao waweze kujifunza kupitia uzoefu wao huku vikundi vilivyopo vikiimarishwa zaidi”. Amesema Yona.

Baadhi ya washiriki wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kuboresha utendaji wao wa kazi tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo walikuwa wakikumbana na changamoto ya kutambua mazingira halisi yanayowakabili watoto na vijana kupitia klabu zao.

Shirika la AGPAHI kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia taasisi ya Centres for Disease Control (CDC), linashirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutekeleza afua mbalimbali za kupambana na maambukizi ya VVU pamoja na kuwahudumia watu wanaoishi na maambukizi hayo.
Mmoja wa Wawezeshaji, Margaret Safe kutoka Kibaha mkoani Pwani akifafanua jambo kwenye mafunzo hayo.
Mwezeshaji, Margaret Safe akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.
Afisa Miradi, Huduma Unganishi kwa Jamii kutoka shirika la AGPAHI, Cecilia Yona akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com