Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amesema wakati umefika
kwa kamati na bodi za Shule mkoani humo kujitathmini ikiwa zinafaa kuendelea na
majukumu yao au kujiuzulu pale Shule zao zinapofanya vibaya katika ufaulu wa
mitihani ya Taifa.
Mtaka ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Wenyeviti wa
Kamati na Bodi za Shule za Halmashauri ya Mji Bariadi na Halmashauri
ya Wilaya ya Bariadi katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari
Bariadi, katika kikao maalum kilicholenga kujadiliana na
kupanga maandalizi ya Kambi za kitaaluma kwa Kidato cha Nne na Darasa la Saba
Wilayani humo.
Amesema mara nyingi
wanafunzi wanapofanya vibaya kwenye mitihani wazazi wengi wamekuwa wakiwalaumu
na kuwanyoshea vidole walimu badala ya kutathmini mchango wao katika ufaulu wa
watoto wao.
“ Watoto wakifeli
mnaanza kuwanyoshea walimu vidole, huu mwaka watoto wakifeli kamati za shule
zijiuzulu, mnapowanyoshea walimu vidole hivi kamati za shule zenyewe huwa
zinachukua wajibu gani, jiuzuluni ili waje wazazi wengine wenye mawazo mapya
yatakayozivusha shule kwenda kwenye ufaulu mzuri” alisisitiza Mtaka.
Mtaka amewataka wazazi
washikamane na Serikali pamoja na walimu katika kuhakikisha wanafanya mapinduzi
ya Elimu, hivyo akasisitiza kuwa Wenyeviti wa Kamati na Bodi za Shule wakafanye
vikao na wazazi kuweka mipango mizuri ya kufanikisha kambi za kitaaluma kwa
wanafunzi wa kidato cha nne na darasa la saba pamoja na maendeleo ya elimu kwa
ujumla.
Aidha, kama
Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa Mtaka amewahakikishia wazazi
kuwa wanafunzi wote watakaokuwa katika kambi watatunzwa na kulindwa huku
akiwatahadharisha watu wenye nia mbaya kutowafuatilia wanafunzi wa kike kwa
lengo la kuwarubuni kwa namna yoyote kwa kuwa Serikali itawachukulia hatua wote
watakaobainika.
Mtaka amesisitiza
wazazi wote kuchangia mahitaji mbalimbali kwa wanafunzi watakaokuwa kambini ili
kuwezesha kambi hizo kufanyika hususani chakula, huku akiwaeleza wazazi kuwa
kupitia kambi hizo watarajie kuona mabadiliko ya kitaaluma kwa watoto wao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya
Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amezitaka Kamati na Bodi za Shule wilayani humo
kufanya vikao na Wazazi kwa ajili ya kuwaeleza wajibu wao katika kufanikisha
Kambi hizo za Kitaalamu na kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo Mei
30, 2018 ofisini kwake.
Kiswaga amesema Kamati
zote ambazo zitashindwa kutekeleza agizo hilo zitavunjwa na Wenyeviti na
wajumbe wa Kamati hizo watawajibishwa.
Wilaya ya Bariadi
itazindua rasmi kambi za Kitaaluma kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne
na Darasa la Saba Juni 06 mwaka huu.
MWISHO:
0 comments:
Post a Comment