Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amewahakikishia wazazi
wote mkoani humo kuwa Serikali itawalinda na kuwatunza wanafunzi wote kwa Kidato
cha Nne na Darasa la Saba watakaokuwa katika Kambi za Kitaaluma zinazotarajiwa
kuanza rasmi mapema mwezi Juni 2018 kwa kwa muda wa siku zote 21,
katika mkoa mzima.
Mtaka ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Wenyeviti wa
Kamati na Bodi za Shule katika Shule ya Msingi Mshikamano Wilayani Meatu katika
kikao maalum kilicholenga kujadiliana juu ya maandalizi ya Kambi hizo
Wilayani humo.
Amesema Serikali
imebeba dhamana ya kuwaweka wanafunzi kambini kwa lengo la kuwaandaa
vema ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao na kuongeza ufaulu, hivyo
haitawafumbia macho wale wote watakaoonekana kwa njia moja ama nyingine
kuharibu jitihada hizo.
“Nawaambia hapa
wananchi wa Meatu, kambi za wanafunzi wetu za kitaaluma mziogope kama ukoma,
sisi hatuwezi kubeba dhamana ya watoto wa watu kwenda kwenye makambi halafu aje
mtu anajipitisha pitisha kwenye kambi kufuatilia na kutaka kuwarubuni watoto
wetu wa kike, nawaeleza hapa mtakuwa halali ya polisi” alisema Mtaka.
Ameongeza kuwa wakati
wote wanafunzi watakapokuwa kambini Serikali itawawezesha walimu kupata stahili
zao kutekeleza majukumu yao na kwa kushirikiana na wadau wengine itatoa
mahitaji maalum kwa wanafunzi wa kike, hivyo akawataka wazazi kujiandaa
kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao ambacho ni sehemu ya kile ambacho
kingetumika wakiwa nao nyumbani.
Aidha, Mtaka amewataka
wazazi, walimu kushikamana na Serikali katika kufikia azma ya kufanya mapinduzi
ya Elimu mkoani Simiyu kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake badala ya kuwatupia
lawama walimu pekee kila wanafunzi wanapofanya vibaya katika mitihani yao, kwa
kuwa ufaulu wa mwanafunzi unategemea ushirikiano katika ya walimu,
wazazi na wanafunzi.
Kwa upande wao
Wenyeviti wa Bodi na Kamati za Shule wamepongeza kuwepo kwa kambi hizo za
Kitaaluma na wakakiri kuwa kambi hizo zinaweza kuwa suluhu ya kuondokana na
daraja la nne na sifuri kwa kidato cha nne na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa
darasa la saba na wakatoa maoni yao.
“ Binafsi nampongeza
Mkuu wa mkoa kwa kuja na wazo hili la kufanya makambi ya kitaaluma kwenye mkoa
wetu, napendekeza kambi hizi zisiishie kwenye hizo siku 21 za mwezi wa sita
tu, wazazi tushikamane tuchange chakula watoto wetu wakae kambi hata
mwezi wa tisa” alisema Mchungaji Fabian Kuzenza.
“Naunga mkono kuwepo
makambi ya kitaaluma na namsukuru Mkuu wa Mkoa kuzungumza na
sisi, hii imetusaidia kuwa na uelewa wa pamoja naomba pia atusaidie
wajumbe wetu wa kamati za shule wapewe mafunzo wawe na uelewa mpana wa masuala
mbalimbali, ili wawe wanawaeleza wazazi mambo wanayoyafahamu” Eliasi kamweji
Mwenyekiti Kamati ya Shule ya Msingi Paji.
Mwezi Juni mwaka huu
Wilaya zote mkoani Simiyu zitafungua Kambi za Kitaaluma kwa wanafunzi wa Kidato
cha Nne na Darasa la Saba kwa muda wa siku 21 na katika siku hizo wanafunzi
wote watafanya mtihani wa majaribio kwa ajili ya maandalizi ya Mitihani ya
Kitaifa iliyo mbele yao.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment