Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Joseph Butiku (wa pili kushoto) akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Simiyu, kabla ya kuanza Mdahalo wa uongozi na maendeleo yenye tija kwa wote uliondaliwa na Taasisi hiyo kwa viongozi wa Mkoa wa Simiyu, ambao ulifanyika Machi 11, 2019 Mjini Bariadi(kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Joseph Butiku katika Mdahalo wa uongozi na maendeleo yenye tija kwa wote uliondaliwa na Taasisi hiyo kwa viongozi wa Mkoa wa Simiyu, ambao ulifanyika Machi 11, 2019 Mjini Bariadi.
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera akichangia hoja katika mdahalo wa uongozi na maendeleo yenye tija kwa wote uliondaliwa na Taasisi ya mwalimu Nyerere kwa viongozi wa Mkoa wa Simiyu, ambao ulifanyika Machi 11, 2019 Mjini Bariadi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Joseph Butiku (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu mara baada ya ufunguzi wa mdahalo uliondaliwa wa uongozi na maendeleo yenye tija kwa wote na Taasisi hiyo kwa viongozi wa Mkoa wa Simiyu, ambao ulifanyika Machi 11, 2019 Mjini Bariadi.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa
wito kwa viongozi kutumia nguvu nyingi kujifunza badala ya kutumia nguvu
nyingi kuamua ili wanapofanya maamuzi waamue maamuzi yenye tija kwa maendeleo
ya wananchi katika maeneo yao.
Mtaka amesema hayo Machi 11, 2019 Mjini Bariadi
katika Mdahalo wa uongozi na maendeleo yenye tija kwa wote uliondaliwa na
Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa viongozi wa Mkoa wa Simiyu,ambao uliwashirikisha
viongozi ngazi ya Wilaya na Mkoa.
“Ni vizuri tukatumia nguvu
nyingi kujifunza kuliko kuamua kwa sababu kama hutaki kujifunza unataka uamue
utaamua hata usiyoyajua, inawezekanaje mtu anateuliwa leo kuwa Mkuu wa Mkoa,
Wilaya au Mkurugenzi halafu unakuwa mtaalam wa kila kitu, kilimo wewe, afya
wewe, elimu wewe ; unafikiri unaweza kutranform ( kufanya mabadiliko/mapinduzi
ya) uchumi wa nani?” alisema Mtaka.
Aidha, katika
kumuenzi Mwalimu Nyerere amewaasa viongozi wenzake waliopewa dhamana na Mhe.
Rais kuwatumikia wananchi kushughulika na masuala yanayohusu maendeleo ya
wananchi badala ya kujikita katika mambo yasiyo na tija ikiwemo ugomvi kati
yao.
“Tumeaminiwa na Mhe. Rais
tukapewa dhamana tuwatumikie Watanzania wenzetu tujishughulishe na masuala ya
wananchi tuache mambo yasiyo na tija kwa wananchi; hivi kuna haja gani DC
kugombana na DED au RC kugombana na RAS? Kwa nini tumsumbue Mhe. Rais badala ya
kuongelea masuala ya maendeleo ya wananchi abaki kuzungumzia mambo ya ugomvi wa
viongozi? Alihoji Mtaka
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Bw. Joseph Butiku ametoa wito kwa
viongozi kuheshimu Katibu ya Jamhuri ya Muungano waTanzania na kuishi katika
misingi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika uongozi wao.
Aidha, Butiku ametoa rai
kwa viongozi wote wa Serikali kutumia madaraka waliyopewa kwa maslahi ya
wananchi na wahakikishe wanawafikia wananchi mpaka ngazi za chini ili
waweze kuwasaidia namna bora ya kutumia shughuli za uzalishaji
wanazozifanya hususani kilimo na mifugo kujikwamua kutoka katika umaskini.
Akitoa mada kwa viongozi wa
Mkoa wa Simiyu, Mjumbe kutoka Taasisi ya Mwalimu Nyerere Bw. Gallus Abed
amesema katika kuwaletea maendeleo wananchi ni lazima viongozi wajiwekee
malengo na kusimamia utekelezaji wa malengo hayo na kuhakikisha wanapima
matokeo yake.
Nao baadhi ya Viongozi wa
Mkoa wa Simiyu wakichangia hoja katika mdahalo wa uongozi na maendeleo yenye
tija kwa wote wamezungumzia mchango wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere na namna
wanavyomuenzi Mwalimu Nyerere katika utekelezaji wa shughuli zao za kuwaletea
maendeleo wananchi.
“Tunaishukuru Taasisi ya
Mwalimu Nyerere kwa namna ambavyo imeamua kutufikia na kuendelea kutuonyesha,
kutukumbusha na kuturejesha ili tuishi maisha ya Mwalimu Nyerere ambaye amekuwa
mfano wa kuigwa” Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini.
“Serikali ya awamu ya tano
imekuwa ikiyaishi maono ya Baba wa Taifa, Mwl.Julius Nyerere, kama unavyoona
Mhe. Rais amekuwa akisema na sisi tunaona miradi mikubwa ya maendeleo
inatekelezwa kwa fedha zetu za ndani” Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano
Mwera.
“Tunatekeleza fikra za Mwalimu Nyerere kwa kuanzia
hasa katika utekelezaji wa malengo yaliyoko katika Dira ya Maendeleo ya
Taifa ya Miaka Mitano kwenye maeneo yetu” Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Mji wa Bariadi, Bibi.Suzana Sabuni.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment