Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Vijana Mkoani Morogoro wametakiwa kuchangamkia
fursa za kilimo zilizopo katika Mkoa huo ili kujiwezesha na kujiimarisha
kiuchumi.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary
Mgumba leo tarehe 23 Machi 2019 wakati akizungumza katika uzinduzi wa Jukwaa la
Vijana wa Mkoa wa Morogoro mkutano ulioudhuriwa na Vijana wa Mkoa huo pamoja
viongozi mbalimbali.
Naibu waziri Mgumba amewataka Vijana hao
kuchangamkia fursa hizo ikiwa ni pamoja na kupata mkopo kutoka Benki ya
Maendeleo ya Kilimo (TADB) na mikopo ya Matrekta kutoka Shirika la maendelo la
Taifa (NDC) Mjini Kibaha ili kuweza kujiari katika sekta hiyo.
Amesema kuwa Mkoa wa Morogoro umepata bahati ya
kuwa na viwanda vikubwa ambavyo vinahusika katika sekta ya Kilimo ikiwemo
Kiwanda cha Mtibwa, kilombero, Mkulazi 1 na 2, Mansoor industry cha
kutengeza Sigara, ujenzi wa Kiwanda cha kukoboa Mpunga na Kiwanda cha
kuchakata mazao ya jamii ya Mikunde cha Maharage.
Mhe Mgumba amewataka Vijana kutosubiri ajira za
kuajiwa ofisini na badala yake waungane kwa pamoja kwa kuanzisha mashamba,
kushiriki katika ujasiriamali wa mazao ya kilimo, kutoa huduma kwenye sekta ya
kilimo na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo ili kutengeneza ajira.
Akizungumza na mamia ya Vijana wa Mkoa wa Morogoro
katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Waislamu mkoani Morogoro Naibu waziri wa Kilimo
Mhe Omary Mgumba amewahakikishia Vijana kuwa serikali inayoongozwa na Mhe Rais
Dkt John Pombe Magufuli imedhamiria kuwakomboa wakulima kupitia mazao ya
Kimkakati kupitia Programu kabambe ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili
yaani ASDP II.
Alisema kuwa ni vyema Vijana hao wakashirikiana na
wataalamu mbalimbali ili kuhakikisha wanalima Kilimo chenye tija, na kujiunga
kwenye Vikundi na kuwa na ardhi zenye hati miliki zitakazo tumika kwa ajili ya
uzalishaji mali na kuwa dhamana kwenye taasisi za fedha kupata mitaji ya
kuwekeza kwenye kilimo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt Kebwe
Steven Kebwe amesema kuwa Mkoa huo umebarikiwa kwa kiasi kikubwa kwani asilimia
kubwa ya mazao mbalimbali hustawi vizuri.
Dkt Kebwe amesema kuwa Mkoa huo pia una ardhi kubwa
ambayo inafaa kwa Kilimo ikiwemo cha umwagiliaji kutokana na kuwepo na mito
mingi ambayo itamuwezesha mkulima kulima kwa kipindi chote.
Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuwapongeza Vijana
wanaohitimu chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kwa jitihada zao za kujiingiza
katika Kilimo na kutosubiri ajira za serikali.
Jukwaa la Vijana Mkoa wa Morogoro limezinduliwa na
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe Suleiman Jafo ambapo amewataka Vijana
hao kuhakisha wanatumia vyuo vya Kilimo vilivyopo katika Mkoa huo kubalidisha
hali ya Mkulima.
Jukwaa la Vijana Mkoa wa Morogoro limezinduliwa
likiwa na kauli mbiu "Fursa Zetu Mkoa Wetu"
MWISHO
0 comments:
Post a Comment