Waziri wa Madini Doto Biteko akieleza jambo wakati akifungua kikao kazi cha kupitia na kujadili Mpango Mkakati na Mkakati wa Kibiashara wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC). Wengine ni watendaji wa Wizara na Taasisi.
Waziri wa Madini Doto Biteko katikati kipitia jambo wakati wa kikao kazi cha kupitia na kujadili Mpango Mkakati na Mkakati wa Kibiashara wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC). Kulia ni Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na kushoto ni Katibu Mkuu, Prof. Simon Msanjila.
Mtaalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Dkt. George Mofulu akieleza jambo wakati akiwapitisha wajumbe wa kikao hicho katika mikakati hiyo.
Waziri wa Madini Doto Biteko amezitaka
taasisi zilicho chini ya Wizara kufikiri kibiashara ikiwemo kutafuta njia zitakazowezesha
sekta ya madini kuchangia zaidi katika pato la taifa.
Waziri Biteko ameyasema hayo Machi 23,
jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha kupitia na kujadili Mpango
Mkakati na Mkakati wa Kibiashara wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) iliyoandaliwa
na Wataalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Aidha, amezitaka taasisi hizo kuhama katika
mtindo wa kutegemea ruzuku ya serikali badala yake zijiendeshe kibiashara na
kuwataka watendaji wa wizara na taasisi kuhakikisha wanafanya mageuzi
yatakayowezesha sekta hiyo kuchangia zaidi sambamba na kasi yake ya ukuaji
kiuchumi.
“
Serikali kwa upande wake imeshafanya mageuzi makubwa. Tunataka Idara, kitengo
na taasisi zifanye mageuzi. Tuwe na taasisi ambayo mfanyakazi anaweza kueleza
amefanya nini kipya,” amesisitiza Waziri Biteko.
Pia, ameongeza kuwa, ukataji madini ni suala
ambalo linalopaswa kuchukuliwa kwa uzito wa kipekee kutokana na umuhimu wake katika
biashara ya madini na hususan kipindi hiki ambacho serikali inasisitiza
shughuli za uongezaji thamani madini kufanyika nchini ikiwemo kuhamasisha
ujenzi wa viwanda hivyo.
Vilevile, amewataka washiriki wa kikao
hicho kuwasilisha mawazo chanya yatakayosaidia kuboresha mkakati huo utakopelekea
uboreshaji wa kituo cha TGC.
Aidha, amewataka watendaji wa Kituo cha TGC
kuhakikisha wanakitangaza kituo hicho ikiwemo kuwafanya wachimbaji wadogo wa
madini kuwa marafiki wa kituo hicho.
Kwa upande wake, Naibu wa Waziri wa Madini
Stanslaus Nyongo, amesema serikali iliona umuhimu wa Kituo cha TGC hali ambayo
imepelekea kuandaliwa kwa mikakati hiyo na kueleza kuwa uwepo wake unapaswa
kutoa mabadiliko katika kituo hicho na hususan katika eneo la uongezaji thamani
madini.
Ameongeza
kuwa, uongezaji thamani madini ni jambo ambalo serikali inaliangalia kwa
umuhimu wake na kueleza kuwa ni miongoni mwa mambo yaliyopelekea kufanyika kwa mabadiliko katika
Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na 2017 ili taifa liweze kunufaika zaidi.
Ameeleza masuala mengine yaliyopelekea
serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya madini ni pamoja na kutaka kuongeza
mapato ya serikali yanayotokana na madini, serikali kushiriki katika uchumi wa
madini na kumiliki hisa, kushirikisha jamii katika miradi ya madini na kampuni za
madini kushirikiana na jamii.
Aidha, amewashukuru wataalam washauri Prof.
Beatus Kundi na Prof. Marcellina Chijoriga kutokana na ushauri wao walioutoa
kwa wizara wakati wa kupitia Mikakati hiyo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara
yaMadini, Prof. Simon Msanjila amewataka watendaji wa Wizara kuhakikisha kila
mmoja anaangalia eneo linalomhusu katika kituo hicho na kulifanyia kazi
kikamilifu ili kufikia lengo linalotarajiwa.
Wizara ya Madini iliona umuhimu wa
kukiimarisha Kituo cha TGC ili kijiendeshe kibiashara kutokana na fursa
zilizopo katika sekta ya madini hususan kwenye ukataji wa madini. Pia, kutokana
na fursa zilizopo katika ukataji wa madini ya vito na jimolojia kwa ujumla,
wizara iliona TGC inaweza kujiendesha kibiashara na hivyo kuongeza mapato kwa
serikali.
Kazi ya kuandaa Mikakati hiyo imetekelezwa
kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) na kuandaliwa na Wataalam Elekezi kutoka Chuo
Kikuu cha Mzumbe na kupitiwa kikamilifu na Prof. Beatus Kundi na Prof.
Marcellina Chijoriga kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Watendaji
kutoka Wizarani na taasisi zake.
0 comments:
Post a Comment