*Ni kuhusu vijana waliofaulu darasa la saba
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameutaka
uongozi wa mkoa wa Ruvuma uhakikishe kuwa vijana wote wanaomaliza darasa
la saba kwenye kila Halmashuri za mkoa huo wanakwenda kuanza kidato
cha kwanza.
Aametoa agizo hilo leo (Jumatano, Januari 2, 2018)
wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Ruvuma baada ya kuwasili kwenye
uwanja ndege wa Songea kuanza ziara ya kikazi ya siku nne
mkoani Ruvuma.
Waziri Mkuu amesema Halmashuri zote za
mkoa huo zijikite katika kujenga madarasa ili wanafunzi wote waliofaulu ambao
wanatakiwa kwenda sekondari waende.
Amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa
dhati kuahakikisha kwamba watoto wote wenye sifa za kupata elimu ya seondari
wanapata elimu hiyo kote nchini hivyo juhudi za makusudi lazima zifanywe na
kila Halmashauri ili kutimiza azma.
Akizungumzia suala la utoro shuleni, Waziri Mkuu
amesema hilo ni moja kati ya maeneo yanayozorotesha juhudi kubwa za Serikali za
kuwapatia watoto wa Tanzania elimu katika maeneo mengi
nchini na lazima viongozi wa wilaya na mikoa wasimame imara ili kukomesha hali
hiyo.
Amesema viongozi wa ngazi zote katika mikoa na
wilaya ndiyo hasa wanaoweza kumaliza tatizo la utoro wakishirikiana kwa karibu
na wanavijiji ambao wanaishi na watoto hao na wanajua ni
watoto wangapi hawaendi shule.
Hivyo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kutoa
maelekezo na miongozo itakayowabana watoto watoro pamoja
na wazazi au walezi wao kwani wanayo mamlaka na uwezo wa kuchukuwa
hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.
Akizungumzia zao la korosho , Waziri
Mkuu amewataka viongozi wa mkoa wa Ruvuma kuwaondolea hofu wananchi wanaolima
zao hilo katika mkoa huo kwa kuwahakikishia kwamba Serikali inazo
fedha za kutosha kununua korosho zote ziliyovunwa na wakulima.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato ya Serikali, Waziri
Mkuu amewataka viongozi wa mikoa na wilaya kubeba dhamana waliyopewa
na Taifa ambayo ni pamoja na kusimamia ukusanyaji mapato ya Serikali kwa
kishirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). "Halmashauri zote na
wakuu wa wilaya wasimamie kwa dhati ukusanyuaji wa kodi."
Akiwa mkoani Ruvuma, Waziri Mkuu kesho anatarajiwa
kufungua soko la mazao la Lilambo katika wilaya ya Songea, kufungua ghala la
mazao la Mgazini na kuweka jiwe la msini la ujenzi wa
zahanati ya Luganga na kisha kuhutubia mkutano wa hadhara.
Keshokutwa Waziri Mkuu ataongoza
kikao cha wadau wa zao la kahawa kitakachowashirikisha pia Waziri wa
Kilimo na Mrajisi wa Ushirika. Wengine watakaoshiriki katika kikao
hicho ni viongozi wa AMCOS, UNION na viongozi wa Bodi ya kahawa.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment