METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, January 3, 2019

WAZIRI MKUU ATOA AGIZO KWA VIONGOZI RUVUMA




*Ni kuhusu vijana waliofaulu darasa la saba

Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa mkoa wa Ruvuma uhakikishe  kuwa vijana wote wanaomaliza darasa la saba kwenye kila Halmashuri  za mkoa huo wanakwenda kuanza kidato cha kwanza.

Aametoa agizo hilo leo (Jumatano, Januari 2, 2018) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Ruvuma baada ya kuwasili kwenye uwanja  ndege wa Songea kuanza ziara ya kikazi  ya siku nne mkoani Ruvuma.

 Waziri Mkuu  amesema Halmashuri zote za mkoa huo zijikite katika kujenga madarasa ili wanafunzi wote waliofaulu ambao wanatakiwa kwenda sekondari waende.

Amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa dhati kuahakikisha kwamba watoto wote wenye sifa za kupata elimu ya seondari wanapata elimu hiyo kote nchini hivyo juhudi za makusudi lazima zifanywe na kila Halmashauri ili kutimiza azma.

Akizungumzia suala la utoro shuleni, Waziri Mkuu amesema hilo ni moja kati ya maeneo yanayozorotesha juhudi kubwa za Serikali za kuwapatia  watoto wa Tanzania elimu katika  maeneo mengi nchini na lazima viongozi wa wilaya na mikoa wasimame imara ili kukomesha hali hiyo.

Amesema viongozi wa ngazi zote katika mikoa na wilaya ndiyo hasa wanaoweza kumaliza tatizo la utoro wakishirikiana kwa karibu na wanavijiji ambao wanaishi na watoto hao na wanajua ni watoto  wangapi hawaendi shule.

Hivyo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kutoa maelekezo na miongozo itakayowabana  watoto watoro  pamoja na wazazi au walezi wao kwani wanayo mamlaka  na uwezo wa kuchukuwa hatua  kwa mujibu wa sheria za nchi.

Akizungumzia  zao la korosho , Waziri Mkuu amewataka viongozi wa mkoa wa Ruvuma kuwaondolea hofu wananchi wanaolima zao hilo katika mkoa huo kwa kuwahakikishia  kwamba Serikali inazo fedha za kutosha kununua korosho zote ziliyovunwa na wakulima.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato ya Serikali,  Waziri Mkuu amewataka  viongozi wa mikoa na wilaya kubeba dhamana waliyopewa na Taifa ambayo ni pamoja na kusimamia ukusanyaji mapato ya Serikali kwa kishirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). "Halmashauri zote na wakuu wa wilaya wasimamie kwa dhati ukusanyuaji wa kodi."

Akiwa mkoani Ruvuma, Waziri Mkuu kesho anatarajiwa kufungua soko la mazao la Lilambo katika wilaya ya Songea, kufungua ghala la mazao  la Mgazini na kuweka jiwe la msini la  ujenzi wa zahanati ya  Luganga na kisha kuhutubia mkutano wa hadhara.

Keshokutwa Waziri  Mkuu  ataongoza kikao  cha wadau wa zao la kahawa kitakachowashirikisha pia Waziri wa Kilimo na Mrajisi  wa Ushirika. Wengine watakaoshiriki katika kikao hicho ni  viongozi wa AMCOS, UNION na viongozi wa Bodi ya kahawa.

Mwisho
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com