Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akiangalia moja ya majalada ya ardhi aliyokagua katika halmashauri ya wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma wakati wa uhamasishaji ulipaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi, kushoto kwa waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Vumilia Nyamuga na kulia ni Afisa Ardhi Mteule Letare Shoo.
Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma (hawapo pichani) Mwishoni mwa wiki wakati akihamasisha ulipaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akioneshwa sehemu ndani ya jengo jipya la halmashauri ya wilaya ya Chamwino na Mkuu wa Idara ya ardhi Christopher Sanga alipowasili kukagua ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi, wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Vumilia Nyamuga. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Na Munir Shemweta, DODOMA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline
Mabula amekasirishwa na jinsi halmashauri ya wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma
inavyotunza majalada ya Ardhi katika halmashauri hiyo.
Dkt Mabula alikutana na kadhia hiyo mwishoni mwa wiki
alipotembelea masijala ya ardhi katika halmashauri hiyo akiwa katika mfululizo
wa ziara zake kutembelea halmashauri mbalimbali nchini kuhamasisha ukusanyaji
maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
Dkt Mabula alisema, utunzaji wa majalada ya ardhi katika
halmashauri ya Chamwino hauzingatii taratibu za kutunza majalada jambo
linaloweza kutoa nafasi kwa baadhi ya nyaraka kupotea na wakati mwingine
watumishi wasiokuwa waaminifu kuyahujumu
Wakati wa ukaguzi wa majalada ya ardhi katika halmashauri ya
wilaya ya Chamwino Dkt Mabula alibaini majalada mengi yakiwa hayana maelekezo
kutoka kwa afisa mmoja kwenda kwa mwingine jambo linaloonesha kuwa utendaji
kazi katika sekta hiyo hauna maelekezo yoyote.
‘’mawasiliano ya ofisi lazima yaonekane kutoka kwa ofisa mmoja
kwenda kwa mwingine na hapa kuna index namba lakini haitumiki na huwezi kujua
aliyepokea nyaraka kwa mara ya kwanza nani hapo lazima migogoro isiishe.’’
Alisema Mabuila.
Dkt Mabula alisema, utunzaji majalada ya ardhi usiozingatia
taratibu kwa kiasi kikubwa ndiyo chanzo cha migogoro mingi ya ardhi katika
maeneo mbalimbali kwa kuwa ni rahisi kucheza na majalada kwa nia ya kufanya
udanganyifu.
Naibu waziri wa Ardhi alitoa maagizo kwa Mkuu wa Idara ya Ardhi
Christopher Sanga na Afisa Ardhi Mteule wa halmashauri hiyo ambaye anahudumu
pia wilaya ya Kongwa Letare Shoo kuhakikisha upungufu uliopo katika majalada ya
ardhi yanarekebishwa kabla mwezi machi mwaka huu na ukifika muda huo atarajea
kuona kama maagizo yake yametekelezwa.
Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
ameagiza kufikia machi mwaka huu 2019 viwanja vyote vya halmashauri ya Chamwino
viwe vimepimwa na kupatiwa hati na Mkurugenzi wake ahakikishe halmashauri
inalipa kodi ya pango la ardhi kwa viwanja inavyomiliki.
Pia ameitaka halmashauri ya Chamwino kuhakikisha wadaiwa wote wa
kodi ya pango la ardhi wanapelekewa ilani za madai na watakaoshindwa kutii
wafikishwe kwenye mabaraza ya ardhi na kusisitiza kuwa suala hilo halitakiwi
kufanywa kisiasa ili kuja na matokeo chanya.
Katika hatua nyingine Dkt Mabula aliitaka idara ya ardhi katika
halmashauri wilaya ya Chamwino kuhakikisha hakuna mmiliki wa kiwanja anayejenga
katika halmashauri hiyo bila kuwa na kibali cha ujenzi ili kuepuka ujenzi
holela.
Naibu Waziri Mabula alisema anataka halmashauri ya Chamwino kuwa
na mji uliopangika na mfano kwa halmashauri nyingine na kusisitiza anachotaka
ni wengine kujifunza kwenye halmashauri hiyo hasa ikizingatiwa Ikulu iko Chamwino.
Katika kutekeleza hilo amewataka watumishi wa sekta ya ardhi
katika halmashauri hiyo kuwa na maadili katika kazi zao ili kuepuka utoaji
kiwanja kimoja kwa zaidi ya mtu mmoja jambo linalotokea kwa baadhi ya
halmashauri na kuleta migogoro.
0 comments:
Post a Comment