METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, January 28, 2019

Uganda na Tanzania zakubaliana kumaliza majadiliano ya Bomba la Mafuta mwezi Juni mwaka huu


 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati), Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Irene Muloni (kulia) na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi (kushoto) wakiwa katika kikao cha majumuisho cha Mawaziri wanaohusika na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania kilichofanyika jijini Kampala-Uganda.
Watendaji mbalimbali kutoka nchini Tanzania wakiwa katika kikao cha majumuisho cha Mawaziri wanaohusika na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania kilichofanyika jijini Kampala-Uganda.

Na Teresia Mhagama, Kampala

Serikali za Uganda na Tanzania zimekubaliana kuwa, majadiliano mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa mradi wa Bomba la mafuta Ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Tanga Tanzania yakamilike ifikapo mwezi Juni mwaka huu  ili kuendelea na hatua ya ujenzi wa bomba hilo.

Hayo yalielezwa kwa nyakati tofauti jijini Kampala na Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dkt Medard Kalemani na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Irene Muloni mara baada ya kufanyika kikao cha Mawaziri mbalimbali kutoka Uganda na Tanzania wanaohusika na mradi huo.

“ Kwa ujumla tumejipanga kuwa, majadiliano yote ya mradi na maandalizi mengine ya mradi kati ya pande zote mbili  yakamilike mwezi Juni mwaka huu ili ujenzi wa mradi pia uanze mwezi Juni  na tunataka kukamilisha mradi huu ndani ya miezi 36 mara baada ya ujenzi kuanza,” alisema Dkt Medard Kalemani. 

Dkt Kalemani alisema kuwa,  kwa ujumla, mradi ulishaanza kutekelezwa kwa kufanyika kazi za awali ikiwemo tathmini ya mazingira  ambayo kwa upande wa Tanzania imekamilika na upatikanaji wa eneo kutapojengwa matenki matano yatakayohifadhi mafuta lita laki tano kila moja  mkoani Tanga ambapo taratibu za ujenzi zinaendelea.

Aliongeza kuwa, mradi huo unatekelezwa hatua kwa hatua hivyo kuna kazi zinazoendelea kufanyika wakati  majadiliano yakiendelea ikiwemo kazi za utafiti wa kijiokemia, kijiolojia na kijiotekniko na kuna kazi zitakazofuata baada ya majadiliano kukamilika.

Vilevile alisema kuwa, mara baada ya kumalizika kwa majadiliano kati ya Serikali ya Tanzania na Uganda, hatua itakayofuata ni majadiliano ya kimkataba kati ya Serikali ya Tanzania na wawekezaji wa mradi ambao ni kampuni ya Total E&P  ya Ufaransa, Tullow Oil ya Uingereza na CNOOC ya China na pia  Serikali ya Uganda itafanya  majadiliano husika na wawekezaji hao.

Akizungumzia kikao hicho cha Mawaziri, Dkt Kalemani alisema kuwa, mara baada ya kusainiwa kwa mkataba wa mradi huo mwaka 2017, kulikuwa na masuala mengi ya kujadili lakini katika vikao mbalimbali vya ngazi ya Mawaziri, wameendelea kukubaliana katika masuala mengi yatakayowezesha mradi kusonga mbele.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Irene Muloni alisema kuwa  mazungumzo kati ya pande hizo mbili yamefanyika vizuri na yale waliyokubaliana, kila pande unaenda kuyawasilisha katika uongozi wa juu wa nchi kabla ya kuendelea na hatua nyingine za majadiliano.

“Kwa ujumla kuna majadiliano mbalimbali yaliyo mbele yetu ikiwemo majadiliano kuhusu ubia wa kampuni (shareholding agreement) ambayo tunatarajia yakamilike mwezi Juni ili kuweza kuanza ujenzi wa mradi,” alisema Muloni.

Vilevile alisema kuwa, Timu za Majadiliano ya Kitaifa kutoka Uganda na Tanzania (GNT) bado zina kazi kubwa ya kufanya na wanaamini kuwa wataendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kuwa wananchi wa Uganda na Tanzania wanafurahia mradi huo muhimu.

Mawaziri kutoka Tanzania waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi,  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com