Na Mathias Canal,
Wizara ya Kilimo
Serikali imesema taifa kwa sasa linakabiliwa na upungufu wa
sukari, zaidi ya tani 260,000 ambazo zinapaswa kuwa sehemu ya mahitaji ya
lazima kama nchi.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Omary Mgumba amekiri kuwa upo upungufu
wa sukari ya viwandani tani 155,000 na kwa sukari ya mezani, upungufu ni zaidi
ya tani 105,000.
Mgumba alitoa taarifa kuhusu upungufu huo, wakati alipokwenda
kujionea hali halisi ya uzalishaji wa sukari katika Kiwanda cha Sukari cha TPC
Moshi.
“Tumeanza ziara ya siku sita mikoani kwa kuanzia mkoa wa
Kilimanjaro na kisha tutakwenda mikoa yote inayolima miwa ili kusikiliza, na
kupokea changamoto na kuzitatua kwa pamoja.
“Tutahakikisha tunamaliza upungufu huu wa sukari hapa nchini,
wawekezaji tuelezeni sisi serikali changamoto zinazowakabili wakati wa
uzalishaji ili tukae na kuona njia bora ya utatuzi wake, kuacha mazingira bora
ya uzalishaji.”
Katika ukaguzi huo, Naibu Waziri Mgumba ameongozana na Mkurugenzi
Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Profesa Kenneth Bengesi.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, mkurugenzi huyo ameeleza bayana
kwamba bado mahitaji ya sukari hapa nchini ni makubwa na kuwataka wawekezaji
waliowekeza katika viwanda vya sukari kuitazama fursa hiyo na kuifanyia kazi.
Kutokana na mahitaji hayo, Profesa Bengesi alisema: “Tumeweka
mazingira rafiki ya wawekezaji kuwekeza katika sekta ya sukari, tunawakaribisha
kwa sasa, serikali imedhamiria kuingia katika uchumi wa kati wa viwanda.”
Awali akitoa taarifa ya uzalishaji wa sukari kwa Naibu Waziri
huyo, Ofisa Mtendaji Mkuu na Utawala wa TPC, Jafary Ally, alisema tangu
walipowekeza katika kiwanda hicho wameweza kuongeza uzalishaji kutoka 36,000
hadi kufikia tani 110,000 kwa mwaka.
“Mawazo ya serikali ya kututaka kuzalisha sukari ya viwandani,
tumeyapokea na tutakaa na bodi yetu kuona kama tunaweza kuwekeza katika sekta
hiyo. Hata hivyo, tunaipongeza serikali kwa kuziba mianya yote ya uingizaji
kiholela wa sukari kutoka nje, sasa wawekezaji wana uhakika wa soko,”alieleza
Jafary.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment