Wakulima katika halmashauri ya wilaya ya Nkasi
mkoani Rukwa wameitikia wito wa kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza
zao la kahawa mkoani Rukwa na kuhakikisha wanalima zao hilo kwa wingi ili
kubadili kipato chao na hatimae kushawishi wawekezaji wa kuchakata zao hilo
kuwekeza Mkoani humo ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Zao la kahawa ni miongozi mwa mazao matano ya
kimkakati yanayohimizwa na serikali ya awamu ya tano katika kuinua kipato cha
wananchi pamoja na pato la nchi kwa ujumla.
Wakulima hao wakiongozwa na mkulima mzoefu wa zao
hilo Elias Mwazembe alisema kuwa zao la kahawa linastawi katika mkoa mzima wa
Rukwa hivyo aliushukuru uongozi wa Wilaya pamoja na Mkoa kwa kuendelea
kuwasaidia pale wanapokwama mbali na changamoto aliyoipata mara ya kwanza
alipolima katika hifadhi yam situ wa mfili na kuondolewa na serikali.
“Nilipoona kwenye Mkoa inakubali na kwenye wilaya
ikabidi nije huku (Kijiji cha) Kalundi nikaanzisha kulima mwezi wa tatu nikaona
ile kahawa inastawi vizuri kwahiyo nikaona hapa sio pa kuachilia niendelee na
zao la kilimo lakini sikutulia niliendeleza hamasa kwa watu wengine kuwaambia
kuwa zao la kahawa mkoani Kwetu linakubali ingawa changamoto ikawa mtu alikuwa
anahitaji avune kwa mwaka huo huo nikasema mbegu iliyopo ni miaka miwili
unaweza kuvuna kahawa na kwa umri nilionao nitavuna mpaka vitukuu,” alisema.
Nae Afisa kilimo wa Kijiji cha Kalundi Jiasi
Muyunga alikiri kuwa kitendo cha mkulima huyo Elias Mwazembe kufika katika
Kijiji hicho kumepelekea wakulima wengi kutaka kujihusisha na kilimo hicho cha
kahawa baada ya kuona kuwa kinastawi vizuri katika Kijiji hicho na hivyo kutoka
wito kwa maafisa ugani wenzie juu ya kuwasaidia wakulima na kuwakikishia kuwa
zao hilo ndilo litakalokuwa mkombozi.
Kwa upande wake Afisa kilimo wa Halmashauri ya
Wilaya ya Nkasi alisema kuwa baada ya kubaini kwamba kata 18 zilizopo ufipa ya
juu zenye eneo la hekta 48,000 kuwa zinafaa kulima zao hilo hal,mashauri
ilianisha maeneo ya kuanza nayo huku wakishirikiana na kituo cha utafiti
cha Tacri kilichopo Mbimba Wilaya ya Mbozi, ili kujua mbegu
inayofaa katika maeneo hayo na hatimae kuwapeleka wataalamu na wakulima kwenda
kujifunza.
“Mkulima ambaye tumemtembelea leo ndugu Mwazembe ni
mmoja wa wakulima hao ambao nae alikwenda kujifunza Mbimba na baada ya kutoka
huko aliendeleza juhudi za kufanya kilimo hiki cha kahawa na tunae mkulima
mwingine yupo Kijiji cha Kakoma kata ya Namanyere nae pia mepanda kahawa karibu
miche 500 na kitaluni ana miche karibu 12,000 na kuna taasisi zaidi ya sita
ambazo tumepa miche iliyotokana na kilo 100 za mbegu ambapo kila kilo moja
inatoa miche 4000, hivyo tunaamini baada ya miaka mitatu halmashauri itaanza
kuona faida yake,” Alisisitiza.
Aidha Afisa kilimo wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa Ocran
Chengula aliwashauri wakulima wote wanaotarajia kuanza kilimo hicho cha kahawa
kuhakikisha kuwa wanaandaa mashimo mapema na kuweka mbolea ili iweze
kuchangayikana na udongo
“Tunatakiwa kuandaa mashimo mapema, kama unategemea
kupanda mwaka huu maana yake unaze kuandaa mashimo mwezi wa nane ama wa tisa
kwa kuchimba mashimo na kuweka mbolea ili mbolea iweze kuchanganyikana na
udongo ikishaanza mvua mwezi wa kumi na moja ile miche inatakiwa ihamishwe
kwenye mashamba ili mvua itakavyonyesha iweze kushika na kuwa na nguvu zaidi ya
kuweza kukua,” Alifafanua.
Mkoa wa Rukwa unategemea kuwa na miche 1,040,000
ifikapo mwakani inayotokana na kilo 260 za mbegu za kahawa inayopandwa kwenye
vitalu mwaka huu ili kuweza kuisambaza kwa wakulima na taasisi mbalimbali ikiwa
ni kuhamasisha kilimo cha zao hilo pamoja na kuinua kipato cha wananchi, mkoa
na taifa kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment