Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akizungumza alipowasili ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita alipofanya ziara katika mkoa huo jana kufuatilia utekelezaji wa maagizo yake kuhusiana na sekta ya ardhi katika halmashauri za Mji na Wilaya ya Geita.
Na Munir Shemweta, WANMM Geita
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula amekerwa na makusanyo madogo ya mapato
katika halmashauri mbalimbali nchini kupitia kodi ya ardhi.
Akizungumza na watendaji wa sekta ya
ardhi wa Halmashauri za Mji na Wilaya ya Geita jana mkoani Geita alipofanya
ziara ya kushtukiza kufuatilia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa katika
halmashauri hizo, Dk Mabula alisema, mapato ya sekta ya ardhi katika halmashauri
nyingi hayaridhishi na kueleza kuwa halmashauri nyingi mapato yake yako chini
ya asilimia 30.
Alisema pamoja na halmashauri hizo kuwa
na mapato kidogo kupitia sekta ya ardhi lakini watendaji wake hawaoneshi
jitihada zozote kuhakikisha wanakusanya mapato ya kutosha kupitia sekta hiyo na
hivyo aliwataka watendaji hao kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato kwa
kuwa msisitizo wa serikali ya awamu ya tano ni kukusanya kodi.
‘’Kwa staili hii tutafika kweli? Mna
bahati mbaya sasa watendaji wa sekta ya ardhi katika halmshauri mtakuwa chini
ya wizara moja kwa moja na rais amepiga kelele kuhuisiana na kodi ninyi
mnarelax’’ alisema Dk mabula.
Hata hivyo, Dk Mabula aliisifu
halmashauri ya Mji wa Geita kwa kukusanya mapato kwa zaidi ya asilimia sitini.
Kwa Mujibu wa taarifa ya Halmshauri ya Mji wa Geita, kuanzia mwezi Julai hadi
Oktoba 2018, halmashauri hiyo imekusanya jumla ya shilingi 389,699,937.28 kati
ya milioni 600,000,000 ilizopanga kukusanya.
Kwa upande wake Halmashauri ya Wilaya
ya Geita kupitia, Afisa Ardhi wake Faraja Kaluwa pamoja na halmashauri hiyo
kupewa malengo ya kukusanya milioni 150 lakini kufikia desemba 2018 imefanikiwa
kukusanya shilingi milioni 12,480,500 tu.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi aliwataka wakuu wa idara za ardhi katika halmashauri za Mji
na Wilaya ya Geita kutoa ahadi ya utekelezaji maagizo aliyoyatoa na hatua gani
zichukuliwe kwao iwapo maagizo hayatatekelezwa kwa wakati.
Maagizo aliyoyatoa Dk Mabula ni
kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya kodi ya ardhi, uingizaji viwanja na
mashamba katika mfumo wa kielektronik, utoaji hati za ardhi pamoja na utoaji
hati za Madai (demand notes) kwa wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi.
Aidha, Dk Mabula ameziagiza halmashauri
zote nchini kuhakikisha zinaingiza viwanja na mashamba kwenye mfumo wa malipo
kwa njia ya kielektronik na kutaka kasi ya utoaji hati kuongezeka ili
kuwawezesha wananchi kiuchumi na wakati huo kuiingizia serikali mapato kupitia
kodi ya ardhi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula amezitaka halmashauri
nchini kuhakikisha zinatoa leseni za makazi katika maeneo yenye nyumba
zilizojengwa nje ya urasimishaji na mipango Miji na kueleza kuwa zoezi hizo
linatakiwa kukamilika mwezi machi mwaka huu.
Dk Mabula amezitaka Halmashauri
kuanisha maeneo yote ya nyumba hizo na kupatiwa leseni za makazi kwa gharama ya
shilingi 5000 sambamba na kuziingiza katika kumbukumbu za halmashauri na
kubainisha kuwa leseni hizo ni hatua za kuelekea wamiliki wake kupatiwa hati.
0 comments:
Post a Comment