Baadhi
ya Wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa maafa ya mkoa wa Rukwa wakiwa katika
Mafunzo ya Usimamizi wa maafa kwa mujibu wa Sheria Na. 7 ya mwaka 2015,
wakati wa mafunzo kwa kamati hiyo mkoani Rukwa.
Kaimu
Katibu Tawala mkoa wa Rukwa, Bi Winnie Kijazi, Mkurugenzi Msaidizi (Utafiti na
Mipango), Ofisi ya Waziri Mkuu, Bashir Taratibu (katikati) na Mratibu wa
Maafa Manispaa ya Sumbawanga wakifuatilia majadiliano wakati wa Mafunzo
ya Usimamizi wa maafa kwa kamati ya maafa mkoani Rukwa.
Na OWM, SUMBAWANGA
Ofisi
ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa, imezishauri Kamati za Usimamizi wa
maafa nchini kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa kuwa na mpango wa Kujiandaa na
kukabili maafa ili kuwa na uwezo wa utayari wa kujiandaa na kukabili
maafa kwa ufanisi.
Akiongea
wakati wa mafunzo kwa Kamati ya Usimamizi ya Maafa ya Mkoa wa Rukwa, juu ya
Usimamizi wa Maafa kwa Mujibu wa Sheria ya Maafa Na. 7 ya mwaka 2015,
Mkurugenzi Msaidizi (Utafiti na Mipango), Ofisi ya Waziri Mkuu, Bashir
Taratibu, alifafanua kuwa Mpango huo ni muhimu kwa kuwa huainisha majukumu na
hatua zitakazochukuliwa na Kamati za maafa kuanzia ngazi ya kijiji,
wilaya na mkoa pamoja na wadau wengine wa maafa.
“Ili
kuweza kukabiliana na maafa pindi yanapotokea na kuhakikisha kuwa wanazuia au
kupunguza athari za maafa yanapotokea kwa ufanisi tumeishauri kamati ya
Usimamizi wa maafa ya mkoa wa Rukwa katika bajeti ijayo watenge bajeti
kwa ajili ya maafa, pia wabuni mbinu za upatikanaji wa rasilimali
zinazohitajika katika usimamizi wa maafa, hili linawezekana iwapo kamati
zote nchini za Usimamizi wa maafa katika ngazi zote zikiwa na Mpango wa
kujiandaa na kukabili maafa” alisisitiza Taratibu
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa maafa ya Mkoa wa Rukwa ,
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Winnie Kijazi, aliihakikishia ofisi ya Waziri
Mkuu kuwa mkoa huo umeamua kuandaa mpango huo kutokana na changamoto walizo
zipata wakati wa maafa ya mvua yenye upepo mkali uliotokea mwishoni mwa
mwaka jana katika halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga na Nkasi.
“Tunaishukuru
Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa kwa uratibu na misaada ya
haraka pindi tulipopata maafa , na sisi tumeamua kuwa na ufanisi katika
usimamizi wa maafa kwa kuandaa Mpango wa Kujiandaa na Kukabili maafa na
tutaelekeza wilaya zote kuandaa mipango yao na kutenga bajeti kwa
ajili ya utekelezaji huo” alifafanua Kijazi
Naye
Mratibu wa maafa mkoani Rukwa Aziza Kalyatiilya alieleza kuwa, tayari wameandaa
Mpango wa kutoa elimu ya Maafa kwa Umma ili kuijengea jamii
uwezo wa kujiandaa, kuzuia, au kukabili na kurejesha hali kwa haraka na ufanisi
pindi maafa yatakapotokea mkoani humo.
Mnamo
mwezi Desemba mwaka jana Halimashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Nkasi mkoani
Rukwa zilipatwa na maafa ya mvua yenye upepo mkali iliyosabaisha vifo,
uharibifu wa mali na Miundo mbinu. Aidha Kamati ya maafa kwa kushirikiana na
Ofisi ya Waziri mkuu, Idara ya Uratibu Maafa, tayari shughuli za kurejesha hali
zinaendelea.
Kwa
mujibu wa sheria ya Usimamizi wa maafa Na. 7 ya mwaka 2015, inaainisha
majukumu ya kamati za usimamizi wa Maafa kuanzia ngazi ya Kijiji hadi
mkoa, ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, jukumu la msingi ni kutafuta rasilimali
kwa ajili ya usimamizi wa maafa katika ngazi husika, pamoja na Kuratibu
na kusimamia shughuli za usimamizi wa maafa na operesheni za dharura ndani ya
Kijiji wilaya au mkoa. Pia kutoa taarifa za tahadhari ndani ya eneo
husika.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment