Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akisalimiana na viongozi wa wilaya ya Chemba mkoani Dodoma alipowasili kwa ajili ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Chemba Simon Odunga.
Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akizungumza na wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Chemba mkoa wa Dodoma alipofanya ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
Na Munir Shemweta, CHEMBA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina
Mabula ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma kupitia upya
uamuzi wake wa kuchukua asilimia sitini wakati wa kutwaa maeneo ya wamiliki
wa Ardhi katika halmashauri hiyo.
Dkt Mabula alitoa kauli hiyo jana akiwa katika mfululizo wa ziara
zake za kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya Serikali kupitia kodi ya Ardhi
katika halamashauri za mkoa wa Dodoma.
Alisema uamuzi uliofanywa na halmashauri ya Chemba kuchukua
asilimia sitini ya eneo na kumuachia mmiliki asilimia arobaini siyo cha
kiungwana na ni cha kinyonyaji ambacho kwa kiasi kikubwa kinamdhulumu mwenye
eneo.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitoa kauli
hiyo baada ya kuelezwa kuwa katika halamashauri hiyo kuna sintofahamu kufuatia
halmashauri kuamua kupima viwanja kwenye eneo la Mapango Mji wa Chemba ambapo
wananchi wasiokuwa na uwezo wa kupima viwanja halmashauri inawapimia kwa
kuchukua asilimia sitini na kuwaachia arobaini.
Alisema, uamuzi wa kuchukua asilimia sitini ya eneo unaofanywa na
halmashauri ya Chemba ni tofauti kabisa na inavyofanyika katika halmashauri
nyingine ambazo zimekuwa zikiwaachia wamiliki asilimia sitini mpaka sabini.
Dkt. Mabula ameitaka halmashauri ya Wilaya ya Chemba kupitia upya
uamuzi wake huo ili kuondoa mgongano baina yake na wananchi ambapo alibainisha
kuwa katika zoezi hilo wamiliki wanaweza pia kuuza maeneo kwa watu wengine
lengo likiwa kupata fedha ya kumilikishwa maeneo yao.
Alisema, pamoja na kuigiza halmashauri hiyo kupitia upya uamuzi
wake lakini pia watendaji wa sekta ya ardhi wanapaswa kutoa elimu kwa wananchi
kuhusiana na zoezi hilo ili kurahisisha upimaji kwa lengo la kuwa na mji
uliopangika.
Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halamashauri ya Wilaya ya Chemba
Enock Mligo alisema halmashauri hiyo kwa sasa inasimamia ukuaji wa Mji wa
Chemba na kupima maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Alisema eneo la Mpango Mji wa Chemba linaundwa na vijiji sita
ambapo shughuli mbalimbali za upangaji wa mji zinatekelezwa kwa mujibu wa
sheria ya Mipango miji na kubainisha kuwa mchakato wa kuvifuta rasmi vijiji
hivyo sita umeshaanza na kuwasilisha maombi Ofisi ya Rais TAMISEMI ili
kuanzisha Mamlaka ya Mji mdogo wa Chemba.
0 comments:
Post a Comment