Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma alipofanya ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda, na wa tatu kushoto ni Mkurugenzi wa Halamashauri ya Wilaya ya Bahi Leo Mavika.
Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akizungumza wakati akikagua mfumo katika ofisi za ardhi halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma alipofanya ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
Na Munir Shemweta, BAHI
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula amekutana na changamoto kubwa
zinazoikabili halmashauri ya wilaya ya Bahi mkoani Dodoma kiasi
cha kushindwa kuwabana maafisa ardhi katika halmashauri hiyo.
Akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha
ukusanyaji maduhuli ya Serikali kupitia sekta ya ardhi katika halmashauri
mbalimbali nchini jana, Dk Mabula aliikuta halmashauri ya Wilaya ya Bahi
ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti na
uhaba wa magari.
Hali hiyo imesababisha halmashauri hiyo
kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kama vile kukusanya maduhuli
ya serikali kupitia sekta ya ardhi, kuwapelekea wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi
hati za madai, kupima na kupanga viwanja pamoja na kwenda kutatua migogoro ya
ardhi.
‘’Sekta ya ardhi ni idara nyeti sana
ambayo inaweza kuingizia seriali mapato mengi lakini kama haitawezeshwa kufanya
kazi ipasavyo kwa kupatiwa rasilimali fedha na vifaa kama magari basi
itashindwa kutekeleza majukumu yake na hivyo kuifanya serikali kukosa mapato
kupitia sekta hiyo.’’ Alisema Dk Mabula
Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya
Wilaya ya Bahi Chediel Mrutu alimwambia Naibu Waziri Mabula kuwa, idara yake
hajawahi kupatiwa fedha za mgao wa ndani na bajeti yake kwa mwaka ni milioni
mbili na laki tano na kubainisha kuwa kiasi hicho wakati
mwingine hakipatikani chote. Kwa mujibu wa Mrutu idara yake haina
gari la kuwawezesha kufanya shughuli za ardhi ambazo wakati mwingine hutakiwa
kwenda umbali mrefu kushughulikia masuala ya ardhi.
Kufuatia hali hiyo Dkt. Mabula alitaka
kufahamu kiasi cha fedha za mgao inazopata idara nyingine kwenye halmashauri
hiyo kufuatia katika ziara zake kubaini idara ya ardhi kutengwa na kupewa kiasi
kidogo cha fedha ukilinganisha na halmashauri nyingine ambapo kwa upande wa
Bahi hakuna tofauti jambo lililomfanya kuishiwa nguvu na kusema halmashauri
hiyo inahitaji kusaidiwa.
Dk Mabula alisema kiasi cha milioni
mbili na laki tano inazopata halmashauri kwa mwaka haiwezi kufanya kitu kwa
idara kama ya ardhi yenye majukumu mengi jambo lililoifanya kukusanya milioni
saba tu hadi kufikia desemba mwaka jana huku ikiwekewa malengo ya milioni 47.
Alisema kwa hali waliyo nayo
halmashauri ya Wilaya ya Bahi haiwezi kufikia asilimia hamsini ya malengo ya
serikali na kuagiza ofisi ya Kamishana Msaidizi Kanda kuangalia namna
itakavyoweza kuisaidia idara ya ardhi angalau iweze kutatua baadhi ya
changamoto.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya
Bahi Leo Mavika alisema halmashauri yake inakabiliwa na changamoto kubwa ya
upatikanaji mapato ambapo alisema kwa sasa inajitahidi kuhakikisha
kiasi kidogo kinachopatikana kinagawanywa kwenye idara zote za halmashauri huku
idara ya ardhi ikipewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake na kuongeza kuwa
halmashauri hiyo kwa sasa ina magari mawili tu jambo linalowawia vigumu
kutekeleza majukumu ya kila siku.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi
Munkunda alisema ili halmashauri yake iweze kutoka ilipo mikakati madhubuti
inahitajika ili kuondokana na hali hiyo ambayo imekuwa ikiwakatisha tama
watumishi kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo kutokana na
changamoto zinazowakabili.
------------------------------------------MWISHO-------------------------------------------------
0 comments:
Post a Comment