Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akisisitiza jambo wakati alipokutana na wajumbe wa Baraza la Biashara Mkoa wa Kigoma, wakati alipofika mkoani humo kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Baraza la Biashara la Taifa, kulia kwake ni Mkuu wa mkoa huo, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga, Katibu Tawala wa mkoa huo, Rashid Mchata na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Kigoma, wakati Waziri alipofika mkoani humo kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Baraza la Biashara la Taifa
Na. OWM, Kigoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama (Mb),
ameitaja mikoa 11 ambayo ilianzisha mabaraza ya Biashara na hadi sasa yako hai
na kubainisha kuwa mikoa mingine ilitekeleza agizo la kuanzisha mabaraza hayo
tulakini utendaji wa Mabaraza
hayo umekuwa siyo endelevu.
Waziri Mhagama
ameitaja Mikoa hiyo 11 ambayo Mabaraza yake yako hai hadi sasa
kuwa ni Dodoma, Kigoma, Tanga, Geita, Morogoro, shinyanga, Dar es
Salaam, Pwani, Iringa, Songwe na Mbeya. Aidha, Mhagama amebainisha kuwa Mikoa
mingine ambayo mabaraza yake hayafanyi vikao inakiuka Waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2001 unaosisitiza kuanzishwa kwa mabaraza hayo
na utendaji wake kuwa endelevu.
Akiongea wakati wa kufuatilia utekelezaji wa
shughuli za Baraza la Taifa la Biashara mkoani Kigoma, Waziri Mhagama
alifafanua kuwa Dhumuni kuu la
kuanzisha mabaraza ya biashara hususani katika ngazi ya wilaya na mikoa ni
kuweka mfumo rasmi wa kuwakutanisha viongozi wakuu wa Serikali na Sekta Binafsi
katika kila ngazi ya utawala, kujadiliana jinsi ya kuboresha mazingira ya
biashara na uwekezaji nchini kwa ajili ya kukuza sekta binafsi ambayo ndio
muhimili muhimu wa kukuza uchumi wa nchi.
“Hatuwezi kuwa tunamshuhudia Mhe. Rais wa awamu ya
tano Dkt. John Pombe Magufuli anaitisha vikao vya Baraza la Taifa la
Biashara katika ngazi ya Taifa lakini katika ngazi ya mkoa na wilaya
hamtekelezi maagizo hayo, lazima mabaraza yakutane ili kutatua kero za
wafanyabiashara na wawekezaji katika ngazi ya mkoa na wilaya, lakini pia
itasaidia kuibua fursa za uwekezaji na kuzinadi fursa hizo, na sisi tumeamua
kukagua mkoa mmoja baada ya mwingine ili kupunguza kero za wafanya biashara na
wawekezaji” Amesema Mhagama
Wakiongea kwa nyakati tofauti wakati
Waziri Mhagama alipokutana na Wajumbe wa Baraza la Mkoa la Biashara, Mkuu wa
mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga , Mkuu wa wilaya ya
Kigoma, Samson Anga na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Rashid Mchata, walieleza
kuwa kupitia Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji
(LIC), wameweza kuimarisha mfumo wa majadiliano kati ya serikali na sekta
binafsi kupitia Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya.
Naye
Mratibu wa Mradi huo, Andrew Mhina alibainisha kuwa Mradi huo unalenga
kuhakikisha kuwa unaboresha mazingira ya Biashara na uwekezaji nchini
tayari kwa kushirikiana Baraza la Taifa la Biashara wameandaa mwongozo wa
Majadiliano Kati ya Serikali na Sekta Binafsi ngazi ya Mkoa na Wilaya ili
kuyajengea uwezo Mabaraza ya Mikoa yaweze kuwa endelevu na yenye ufanisi.
Baraza
la Taifa la Biashara lilianzishwa kwa Waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2001 na
kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 39 la tarehe 28 Septemba
2001. Baraza
hilo ni jukwaa la majadiliano kati ya Sekta ya Umma na
Sekta Binafsi, na lengo kuu la Baraza ni kuboresha mazingira ya biashara na
uwekezaji kwa njia ya majadiliano kati ya sekta ya umma na sekta
binafsi.Aidha Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la
Biashara ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment