METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, December 8, 2018

“MWANAMITINDO LUCY CHARLES AELEZA NDOTO YAKE KWA JAMII BAADA YA KUTUNUKIWA TUZO YA MWANAMITINDO BORA WA KIKE 2018”

Mapema leo 08/12/2018 Mwanamitindo Lucy Charles amehojiwa katika kipindi cha Jambo Tanzania-TBC 1 ambapo pamoja na mambo mengine ameeleza kiu yake ya kutaka kuwainua wasichana wenye ndoto za kupitia tasnia za Urembo na Uanamitindo. Akiendelea na mahojiano hayo, Mwanamitindo Lucy amesema;

Uanamitindo unalipa endapo utajiweka vizuri katika muonekano, kuishi vizuri kwenye jamii na ukafanya matendo ambayo kampuni yeyote inaweza ikakuamini na kukufanya kuwa balozi pamoja na kuwa na bidii, juhudi na ukajua kwa nini unafanya.

Akielezea sababu ya kuchaguliwa na Swahili Fashion Week kuwania Tuzo, Mwanamitindo Lucy Charles amesema mbali na watu kumchagua katika kipengele alichokuwa akiwania, ushindi huu pia umechochewa na kazi ambazo amezifanya. Mpaka sasa Mwanamitindo Lucy Charles amefanya uigizaji wa Tamthiliya ya Siri za Familia pamoja na Michakato, pia amekuwa Video Vixen ambapo amefanya nyimbo na wasanii mbalimbali kama Ben Pol, Diamond Platnumz, Christian Bella na Eddy Kenzo.

Mwanamitindo anaweza akatangaza bidhaa mbalimbali, anaweza kufanya fashion ili kuonesha kazi ya ubunifu, kutembea Jukwaani(Runway) pamoja na kutangaza nguo au vipodozi vya mbunifu kwenye majukwaa.

Ndoto za Mwanamitindo Lucy Charles ni kuwa ngazi ya kuwasaidia wasichana ambao wanatamani kutimiza ndoto zao kupitia Tasnia ya Urembo na Uanamitindo.

Mwanamitindo Lucy Charles ametoa wito kwa jamii ione kuwa Uanamitindo ni kazi kama kazi zingine hivyo ameziomba familia zibadilishe mtazamo zijikite kukuza vipaji vya watoto na kuvilea tangu wakiwa wadogo.

Hata hivyo Mwanamitindo Lucy Charles ametoa wito kwa wanamitindo wanaoibuka sasa kuwa wajikite kufanya vitu vya asili na waitumie teknolojia kiwasaidia kufikia malengo yao.

Hivi karibuni Disemba 01, 2018 Mwanamitindo Lucy Charles alitunukiwa TUZO ya heshima na kuwa “Mwanamitindo Bora wa Kike wa Mwaka 2018” kupitia Tuzo za Swahili Fashion Week ambazo hutolewa kila mwaka.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com