Waziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda akipata maelezo kutoka Afisa Mradi taasisi ya Milele Zanzibar Eshe Haji Ramadhan katika maonesho ya ujasiriamali yanayoendelea Dar es Salaam katika viwanja vya city Garden Gerezani Dar es Salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda akinunua bidhaa ya unga wa muhogo kutoka mjasiriamali kijana Zaheer Mfaume wa kampuni ya RUM-Zahrain wakati wa maonesho ya ujasiriamali na semina ya ajira katika viwanja vya City Garden Gerezani Dar es Salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa taasisi zilizoshiriki kuandaa semina ya ajira na maonesho ya ujasiriamali kupitia program ya GET HIRED kwa udhamini wa taasisi ya kimataifa ya NAMA Foundation ya nchini Malaysia yanayofanyika viwanja vya City Garden Gerezani Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa viwanda na Biashara Joseph Kakunda amewataka wazalishaji wa bidhaa
mbalimbali nchini kuzingatia ubora wa bidhaa kwa kuangalia viwango vya
kimataifa na kitaifa wakati wa kusambaza bidhaa zao.
Waziri Kakunda alisema hayo leo tarehe 22 Disemba 2018 wakati akifungua semina
ya ajira pamoja na maonesho ya ujasiriamali yaliyoandaliwa kwa pamoja na
taasisi za AN NAHL, TAMPRO, TAMSIA, UKUEM na Pamoja Foundation kupitia program
ya GET HIRED kwa udhamini wa Taasisi ya kimataifa ya NAMA Foundation ya nchini
Malaysia yanayofanyika jijini Dar es Salaam.
Alisema, wafanyabiashara wa Tanzania ni lazima waelewe viwango vya
kimatiaifa wakati wa kuzalisha bidhaa zao kwani mbali na kunufaika na ubora wa
bidhaa lakini pia watakuwa wanaitangaza nchi na uzalishaji bidhaa wowote usio
na ubora wanaopaswa kuwajibika ni wao.
Waziri wa Viwanda na Biashara alibainisha kuwa,kwa Tanzania kuna vyombo
vinavyoangalia ubora wa bidhaa na kuvitaja kuwa ni shirika la viwango
Tanzania ( TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na kusisitiza kuwa
ili wafanyaiashara wafanye kazi kwa ufanisi wanapaswa kuzingatia masharti
ya vyombo hivyo.
Hata hivyo, Kakunda alisema jukumu la kutangaza bidhaa
inayozalishwa ni la wafanyabiashara na hivyo kuwataka kuhakikisha bidhaa
zinakuwa na Msimbohuria (Barcode) kwa lengo la kutambulisha sehemu bidhaa
ilipotoka ama kuzalishwa.
Kwa mujibu wa Kakunda, kukosekana kwa Barcode katika bidhaa za Tanzania
kumesababisha baadhi ya wafanyabiashara wa nchi jirani kutumia mwanya huo
kuonesha kama bidhaa hizo zimetengenezwa katika nchi hizo jambo linalofanya
Tanzania kushuka katika soko la kimataifa.
Alisema, Tanzania imekuwa ikishuka katika soko la AGOA kadri miaka
inavyokwenda na kufikia chini ya asilimia nne kutokana na kushindwa
kujitangaza kimataifa wakati inazalisha bidhaa zenye ubora.
Kakunda alibainisha kuwa, kipaumbele cha serikali ya awamu ya tano kwa
sasa ni kuwa na viwanda vinavyosindika mazao ya kilimo kwa kuwa asilimia 70 ya
watanzania wanajishughulisha na kilimo.
Kwa mujibu wa Kakunda, vipaumbele vingine ni viwanda vinavyoajiri wanachi wengi
kama elfu moja pamoja na viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumika
majumbani kama vile mafuta ya kula, dawa za binadamu, chumvi sukari, unga
maendeleo nguo.
Akielezea mafunzo ya ajira na maonesho ya ujasiriamali, Kakunda alisema
kuwa vijana ni hazina ya kesho hivyo kuna kila jitihada za kuhakikisha nguvu
kazi ya vijana haikumbani na kizuizi chochote kitakachowachelewesha
kufikia malengo.
"Ni lazima tulinde kazi za vijana na wasiwekewe vigingi visivyo na
maana na kama kuna figisu yoyote basi sisi kama serikali tuhakikishe
inaondolewa" alisema Kakunda.
Awali Mwenyekiti wa Taasisi ya AN NAHL Injinia Ally Shaban Kilima alieleza kuwa
semina ya ajira na maonesho ya ujasiriamali inayofanyika yana lengo la
kuwapatia ujuzi vijana waliomaliza vyuo kuwa na ari ya kujiajiri na suala hilo
limechagizwa na juhudi za serikali ya awamu ya tano kuelekea uchumi
wa kati na Tanzania ya viwanda.
Alisema juhudi za taasisi zilizoandaa semina na maonesho ya
ujasiriamali ni kutekeleza ibara ya nane hadi kumi ya ilani ya CCM
kuhusiana na masuala ya ajira kwa vijana.
Mmoja wa vijana anayeshiriki maonesho hayo Zaheer Mfaume kutoka
RUM-Zahrain Investment inayozalisha unga wa Muhogo alisema maonesho
yanayofanyika yanasaidia kutangaza bidhaa wanayozalisha. Hata hivyo alielezea
changamoto kubwa inayowakabili kuwa ni uhaba wa masoko na
kuiomba serikali kusaidia kuwatafutia masoko.
-----------MWISHO--------------
0 comments:
Post a Comment