METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, November 10, 2018

WIZARA YA MADINI, MKANDARASI SUMAJKT WAJADILI MAENDELEO UJENZI WA VITUO VYA UMAHIRI


Waziri wa Madini Angellah Kairuki(katikati) Naibu Waziri Stanslaus Nyongo (kulia) na Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko wakifuatilia kikao  kati ya wizara  na Mkandarasi SUMAJKT anayejega vituo vya umahiri maeneo mbalimbali nchini na Washauri Elekezi Kampuni za Y&P Architects, InterConsult Architects, Sky Architects zinazosimamia ujenzi wa vituo hivyo. Kikao hicho kilijadili maendeleo ya ujenzi wa vituo hivyo.


Sehemu ya Menejimenti ya Wizara wakifuatilia kikao hicho.

Na Asteria Muhozya, Dodoma

Waziri wa Madini Angellah Kairuki tarehe Novemba 8, aliongoza kikao cha kujadili Maendeleo ya Ujenzi wa Vituo vya Umahiri vinavyojengwa maeneo mbalimbali nchini.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Mawaziri Stanslaus Nyongo na Doto Biteko pamoja na Menejimenti ya Wizara ambapo Mkandarasi SUMAJKT na Washauri Elekezi kampuni za Y&P Architects, InterConsult Architects, Sky Architects zinazosimamia ujezi wa vituo hivyo walieleza kuhusu hatua mbalimbali zilizofikiwa za ujenzi wa vituo hivyo.

Vituo vya umahiri vinajengwa maeneo ya mbalimbali nchini kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) ulio chini ya wizara.

Vituo hivyo vinalenga katika kutoa mafunzo ya jiolojia katika utafiti wa madini, mafunzo ya uchenjuaji wa madini kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira hususan kemikali zisizotumia zebaki.

Vilevile, vinalenga katika kutoa mafunzo ya biashara kwa wachimbaji wadogo wa madini, mafunzo ya usalama na afya sehemu za kazi na mafunzo ya namna bora za utunzaji wa mazingira kwenye migodi ya wachimbaji.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki alisisitiza kuhusu kuzingatiwa kwa ubora wakati wa  ujenzi wa vituo husika na kusisitiza Mkandarasi SUMAJKT kukamilisha ujenzi huo katika muda uliopangwa.

Vituo vya umahiri viko katika hatua mbalimbali za ujenzi na vinajengwa Bariadi, Bukoba, Handeni, Musoma, Songea, Chunya, Mpanda na Chuo Cha Madini Dodoma.

Ujenzi wa vituo hivyo utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 11.9 zinazotokana na mkopo wa Benki ya Dunia.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com