Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa
Mtendaji Mkuu wa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA Bi Vumilia L. Zikankuba
Na Mathias Canal-NFRA, Dodoma
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa amefanya
ziara ya kikazi kwa kutembelea na kujionea shughuli zinazofanywa na Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Jijini Dodoma.
Katika ziara hiyo Mhe Bashungwa amekagua ujenzi wa
Maghala na Vihenge vya Kisasa (Silos) ambapo ameipongeza serikali ya awamu ya
Tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kuanzisha ujenzi wa
mradi huo utakaoongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka.
Akizungumza na
wafanyakazi wa NFRA mara baada ya kuzuru katika ofisi hizo zilizopo Mtaa wa
Relini-Kizota Mhe Bashungwa alisema kuwa uongozi imara wa Dkt Magufuli
umepelekea Serikali ya Tanzania na Serikali ya Poland kusaini mkataba wa mkopo
wa masharti nafuu Septemba 2015 wa Dola milioni 55 sawa na sh. bilioni 124, kwa
ajili ya ujenzi wa mradi huo, ambao utaongeza uwezo wa hifadhi ya chakula.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo
ametoa rai kwa Mtendaji Mkuu wa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA Bi
Vumilia L. Zikankuba kuweka msisitizo zaidi katika utoaji elimu kwa wakulima
kuhusu njia bora za kuhifadhi mahindi ili wakati wanapotafuta soko waweze
kupata soko imara na tija kutokana na nafaka hiyo.
Alisema kuwa teknolojia hiyo ni muhimu katika
kipindi hiki ambacho serikali imeamua kwa dhati kuimarisha vyama vya Ushirika
nchini ili kuwa na kauli ya pamoja hivyo wakulima wanapaswa kuwa na Imani na
serikali yao wakati inatekeleza mikakati mbalimbali katika sekta ya kilimo.
Mhe Bashungwa alisema kuwa serikali inatazama
namna nyingine ya Kujenga maghala na vihenge vya kisasa kwa ajili ya mazao
mengine ambayo yapo chini ya Ushirika ili kuimarishwa Zaidi sekta ya kilimo
nchini.
“Ujenzi huu unatufundisha kwamba tunaweza
kujenga maghala katika maeneo mengine nchini hususani katika mikoa ya Lindi na
Mtwara kwa ajili ya zao la Korosho” Alikaririwa Mhe Bashungwa
Mhe Bashungwa ameipongeza NFRA kwa kazi kubwa
ya usimaizi wa ujenzi wa mradi huo ambao umefikia katika hatua nzuri za ujenzi
huku akisisitiza NFRA kupitia idara ya masoko kupunguza mazao ambayo yamekaa
kwa muda mrefu ghalani kuyauza ili fedha hizo zinunue mahindi mengine kwa
wakulima.
Sambamba na hilo Mhe Bashungwa ameipongeza pia
NFRA kwa kununua mahindi ya wakulima kupitia mfumo wa Ushirika katika sehemu
mbalimbali nchini kwa ajili ya kuhifadhi kwani jambo hilo linawanufaisha
wakulima wengi nchini.
“Na katika hili nazitaka Taasisi zingine kuja
kujifunza kwa NFRA kuhusu namna bora ya ukusanyaji wa mazao kwa wakulima”
Alisema
Utekelezaji wa mikataba kati ya NFRA na
wakandarasi ulianza Desemba 2017 ambapo muda wa utekelezaji ni miezi 18 tangu
tarehe rasmi ya kuanza utekelezaji wa mikataba ya wakandarasi, hivyo kabla ya
2020 utakuwa umekamilika.
Ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa (Silos) unatekelezwa
na kampuni mbili za Kandarasi kutoka Poland ambazo ni (Feerum S.A na Unia Araj
Realizacje Sp.o.o) ambapo msimamizi wa utekelezaji wa mradi ni Wakala wa
Majengo Tanzania (TBA) ukihusisha ujenzi wa vihenge vya kisasa, maghala ya
kisasa pamoja na ukarabati wa ofisi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA Bi Vumilia L. Zikankuba alisema kuwa Mradi huo
utaifanya serikali kuwa na uwezo wa kuhifadhi mara mbili ya uhifadhi wa sasa kutoka Tani 251,000 hadi
Tani 700,000 ifikapo mwaka 2025.
Bi Zikankuba ameeleza kuwa Mradi huo utagharimu Dola
za Kimarekani Milioni 55, ikiwa ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya
Poland ikiwa ni sehemu ya kiasi cha milioni 110 kilichotolewa kwa serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, amesisitiza kuwa mikataba ya ujenzi ilianza
kufanya kazi tarehe 9 Disemba 2017 huku akisema Mradi huo utatekelezwa na
kampuni mbili za Kandarasi kutoka Poland ambazo ni (Feerum S.A na Unia Araj
Realizacje Sp.o.o) ambapo msimamizi wa utekelezaji wa mradi ni Wakala wa
Majengo Tanzania (TBA).
Bi Zikankuba alisema kuwa Mradi utahusisha ujenzi wa
vihenge vya kisasa, maghala ya kisasa pamoja na ukarabati wa ofisi na
kutekelezwa katika maeneo nane ambayo ni Arusha (Babati), Dodoma, Makambako,
Mbozi, Shinyanga, Songea, Sumbawanga na Mpanda.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment