Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Isack Kamwelwe akikata
utepe wa boksi lililohifadhi funguo zote za madarasa 24 za shule ya Msingi
Tumaini ya Bukoba, ambapo jana aliikabidhi kwa rasmi kwa Mkuu wa Mkoa wa
Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli. Shule hiyo imejengwana Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Na Mwandishi Wetu, Bukoba
UBORA wa majengo ya shule mpya ya Msingi ya
Tumaini Bukoba yenye miundombinu ya kisasa pamoja na maji na umeme, yataongeza
ufaulu wa wanafunzi wa darasa la Saba, imeelezwa.
Kauli hiyo, imetolewa jana na Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe Isack Kamwelwe alipokuwa akiikabidhi shule
hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti kwa niaba ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe, John Pombe Magufuli.
Mhe. Kamwelwe amesema majengo hayo ya kisasa
yaliyojengwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), ni kielelezo cha
kuwafanya wanafunzi wasome kwa bidii kutokana na kuwa na miundombinu rafiki.
“Hii shule inamajengo mazuri sana natamani
nirudi katika umri wa mtoto ili nisome hapa, maana madarasa mazuri, nasikia pia
kuna umeme na maji ya kutosha, basi ninaimani kubwa ubora huu utakuwa chachu ya
kuongeza juhudi katika masomo na mtafaulu zaidi,” amesema.
Pia amewapongeza TAA kwa kuhakikisha wanawajali
wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kujenga madarasa matatu kwa ajili ya
kufundishiwa na chumba kimoja kinachotumika na walemavu hao kupumzika nyakati
za mchana.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard
Mayongela amesema Mamlaka ilijenga shule hii mpya kwa sababu shule ya zamani ilikuwa
imejengwa eneo hatarishi ikiwa na mita chache kutoka kwenye barabara ya kutua
na kuruka kwa ndege na pia kelele na mingurumo ya ndege sio salama kwa
wanafunzi na walimu wao.
Bw. Mayongela amesema ujenzi wa shule hiyo
imejumuisha jumla ya madarasa 24 kati ya hayo matatu ni ya watoto wenye uhitaji
maalum, jengo la utawala, chumba cha kupumzikia watoto wenye uhitaji maalumu,
uzio na vyoo.
“Kiusalama ilikuwa lazima shule ya Tumaini
iondoke pale kiwanjani na kutafutiwa sehemu nyingine, kwani wakati ndege inatua
inakuwa na makelele na kutua kwake inakuwa karibu na paa la shule inaleta
shida,” amesema Bw. Mayongela.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya TAA,
Mhandisi Prof. Ninatubu Lema amewataka watoto wasome kwa bidii ili waweze
kufika Chuo Kikuu kusomea uhandisi ambao wanahitajika kwa wingi.
“Mimi ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, natamani sana baada ya miaka 15 nije kuwafundisha uhandisi kule Chuo
Kikuu, taifa linauhitaji sana wa Wahandisi, hivyo msome kwa bidii maana hata
shule hii mliyokabidhiwa ni nzuri na inawavutia kusoma, nawapongeza na wazazi
waliowaleta shule kusoma,” amesema Prof. Lema.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali
Marco Gaguti ameishukuru serikali kwa kuwezesha ujenzi wa shule hii, ambayo imejengwa
kwa kuhudumia wanafunzi wazima na wenye mahitaji maalum, ambapo kwa mkoa mzima
hii ndio ya kipekee.
“Tunakuomba ufikishe salaam zetu za shukrani
kwa Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa shule hii, ambayo itainua kiwango cha
elimu cha mkoa wetu, mwaka huu darasa la Saba tumeshika nafasi ya Tano Kitaifa,
ninaimani mwakani (2019) tutakuwa juu zaidi,” amesema.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo,
Bi.Augustina Daniel amesema ufaulu umeongezeka mara dufu na wazazi wamekuwa na
mwamko wa kuandikisha wanafunzi wengi wa darasa la kwanza .
“Tumekuwa tukipata idadi kubwa ya wanafunzi
wanaokuja kujiunga na darasa la kwanza, ambapo mwaka 2018 tumeandikisha 246 wa
darasa la kwanza, na hata ufaulu wa darasa la saba umeongezeka tumefaulisha
kwa asilimia 97.7,” amesema Bi. Daniel.
Shule hiyo yenye wanafunzi 1232 kati ya hao 45
ni wenye uhitaji maalum, na imejengwa na Kampuni ya Ujenzi ya CMG Construction
Co Ltd.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment