Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la Msingi la
Kiwanda cha Kuchenjua Dhahabu cha Nyamigogo wilayani
Nyang'hwale Novemba 28, 2018. Wapili kulia ni mmiliki wa kiwanda hicho,
Hussein Nassoro Amali ambaye pia ni Mbunge wa Nyang'hwale. Wengine pichani
kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constatine Kanyasu,
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mwita Waitara na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi
Robert Gabriel. Watatu kulia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Geita, Alhaj Saidi
Kalidushi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea kiwanda cha Kuchenjua Dhahabu cha Nyamigogo wilayani Nyang'hwale Novemba 28, 2018. Kushoto kwake ni mmiliki wa kiwanda hicho, Hussein Nassoro Amali ambaye pia ni Mbunge wa Nyang'hwale. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama eneo maalum la kuhifadhi na kusafisha Maji machafu wakati alipozindua Kiwanda cha Kuchenjua Dhahabu cha Nyamigogo wilayani Nyang'hwale Novemba 28, 2018. Wapili kushoto ni mmiliki wa kiwanda hicho, Hussein Nassoro Amali ambaye pia ni Mbunge wa Nyang'hwale. Kushoto ni Mke wa Mbunge huyo, Ashura Muhoja. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*Waziri
Mkuu aagiza kuchukuliwa hatua kwa watumishi wote waliohusika
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa ameagiza watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyangw’ale
waliohusika na ubadhilifu wa zaidi ya sh. bilioni tatu fedha ambazo zilitolewa
na Serikali kugharamia miradi ya maendeleo wachukuliwe hatua.
Pia ameagiza kukamatwa na
kuchukuliwa hatua kwa Mkaguzi wa Ndani wa halmashauri hiyo, Gavana Matesa kwa
sababu ameshindwa kutoa kwa mamlaka husika kuhusu taarifa za wizi wa fedha za
maendeleo zilizotafunwa.
Waziri Mkuu ametoa maagizo
hayo leo (Jumatano, Novemba 28, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri
ya wilaya ya Nyangw’ale akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani
Geita.
Miongoni mwa miradi ambayo
fedha zake zimepotea ni pamoja na sh. bilioni 1.2 za ujenzi ofisi ya
halmashauri hiyo, sh. milioni 400 za ukarabati wa kituo cha afya Nyangw’ale,
sh. milioni 611.230 za miradi ya maji.
Nyingine ni sh. milioni
536.119 za mpango wa malipo kulingana na huduma (EP4R), sh. milioni 125.914 za
ushuru wa huduma, sh. milioni 31 za ujenzi wa ofisi ya mbunge na sh. milioni
109 za mfuko wa barabara.
“Wilaya ya Nyangw’ale ni
mpya na Serikali imekuwa ikileta fedha nyingi lakini fedha zote zimetafunwa,
Serikali ipo makini sana na moja kati ya vita kubwa ni dhidi ya mafisadi, wala
rushwa ambayo ni endelevu hivyo tutashughulika na kila mmoja.
Tayari watu saba akiwemo
aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nyangw’ale, Carlos
Gwamagobe na wenzake wamekamatwa. Wizi unatisha Nyangw’ale wilaya inatia aibu
tutawaondoa watu wote waliohusika na tutaendelea kuwakamata.”
Hata hivyo Waziri Mkuu
amewahakikishia wananchi wa wilaya hiyo kwamba Serikali itahakikisha miradi
yote iliyoahidiwa kujengwa kwenye wilaya hiyo ikiwemo ya maji itatekelezwa kama
ilivyopangwa, waendelee kuwa na imani na Serikali yao.
Kuhusua suala la watumishi,
amesema wilaya hiyo lazima iwe na watumishi wasafi wenye weledi wa kufanya kazi
na lazima wahakikishe fedha za miradi zinazotolewa katika halmashauri hiyo
zinalingana na thamani halisi ya mradi.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert
Gabriel amesema atahakikisha watumishi wote wa umma waliohusika na wizi huo
wanachukuliwa hatua stahili na kwamba tayari baadhi yao wameshafikishwa kwenye
vyombo vya dola.
Amesema
halmashauri ya wilaya ya Nyangw’ale inaongoza kwa matumizi mabaya ya fedha za
maendeleo kwa kuwa awali lilikuwa chaka kubwa la wizi, ambapo amesema ni bora
watumishi wote wasiokuwa waadifu waondolewe na waletwe wengine.
Mkuu
huyo wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Gabriel amesema tayari baadhi ya watumishi
wanaotuhumiwa kuhusika katika ubadhilifu wa fedha za miradi mbalimbali
wameshakabidhiwa kwa vyombo vya dola huku watumishi wengine wakiendelea
kuchunguzwa.”Watumishi wote waliohusika na wizi huu watapata tabu sana”
(mwisho)
0 comments:
Post a Comment