METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, November 28, 2018

Majaliwa aanza na wanaotuhumiwa kutafuna mabilioni ya fedha wilayani Nyang'hwale

Na George Binagi-GB Pazzo
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameagiza watumishi wote waliohusika na ubadhilifu wa zaidi ya shilingi bilioni tatu katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Aidha Mhe. Majaliwa ameagiza Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri hiyo, Gavana Mateso akamatwe kwa kushindwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika baada ya kuwepo harufu ya ubadhilifu wa fedha za maendeleo ikiwemo mradi wa maji Nyamtukuza ambao tangu mwaka 2014 hadi sasa haujakamilika.

Baadhi ya fedha za miradi ambayo inaelezwa kuwa na harufu ya ubadhilifu ni pamoja na shilingi bilioni 1.2 za ujenzi wa ofisi ya halmashauri ya Nyang’hwale, shilingi milioni 400 za ukarabati wa Kituo cha Afya Nyang’hwale, shilingi milioni 611.230 za mradi wa maji, shilingi milioni 536.119 za mpango wa malipo kulingana na huduma (EP4R), shilingi milioni 125.914 za ushuru wa huduma, milioni 109 za mfuko wa barabara na shilingi milioni 31 za ujenzi wa ofisi ya mbunge.

Tayari watumishi saba akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang’hwale, Carlos Gwamagobe wamekamatwa kwa ajili ya uchunguzi kuhusiana na ubadhilifu huo. Mhe. Majaliwa yuko mkoani Geita kwa ziara ya kikazi ya siku nne aliyoianza juzi Novemba 27, 2018.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na wakazi wa Nyang'hwale kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Sabasaba.
Baadhi ya wakazi wa Nyang'hwale wakimsikiliza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa (hayuko pichani).
Tazama Video hapa chini
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com