METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, November 27, 2018

BODI YA MWAUWASA YAFANYA ZIARA DUWASA, IRUWASA NA MBEYA UWSA


Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi MWAUWASA na wenyeji wao Mbeya UWSA walipotembelea chanzo cha maji cha Ivumwe.
Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi MWAUWASA na wenyeji wao Mbeya UWSA walipotembelea chanzo cha maji cha Nzovwe. Wa tatu kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi MWAUWASA, Christopher Gachuma.
Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi MWAUWASA na wenyeji wao Mbeya UWSA walipotembelea eneo la kutibu maji la Swaya Jijini Mbeya. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji MWAUWASA, Mhandisi Anthony Sanga. 

Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) imefanya ziara ya siku tano kwenye mamlaka tatu za maji ambazo ni Dodoma (DUWASA), Iringa (IRUWASA) na Mbeya UWSA lengo likiwa ni kujifunza na kubadilishana uzoefu.

Ziara hiyo ilianzia Mamlaka ya Maji Dodoma (DUWASA) na ilihitimishwa kwa kutembelea Mamlaka ya Maji Mbeya UWSA ambapo wajumbe walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya mnyororo mzima wa utoaji huduma ya maji ambayo ni kuanzia kwenye vyanzo vya maji hadi kwa mtumiaji wa mwisho.

Aidha, masuala mbalimbali yalijadiliwa kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kutafuta ufumbuzi wa pamoja wa changamoto zinazozikabili mamlaka za maji nchini ili kufikia azma ya kupanua wigo wa usambazaji wa majisafi na salama kwa wananchi.

Kwa nyakati tofauti, katika majadiliano baina ya wajumbe wa MWAUWASA na wenyeji wao, ilipendekezwa mamlaka ziandae utaratibu wa kubadilishana uzoefu katika utekekezaji wa shughuli zao ili kuleta ufanisi zaidi hasa ikizingatiwa kwamba baadhi ya changamoto kwenye utekelezaji wa miradi ya maji kote nchini zinafanana.

Majadiliano hayo vilevile yaligusia suala zima la wizi wa mita za maji ambao umezikumba mamlaka nyingi nchini na huku baadhi ya mamlaka zikionyesha kufanikiwa kuliko zingine na hivyo ilipendekezwa watumishi wajikite katika suala hili ili kuona ni namna gani wengine wamefanikiwa.

Ziara hiyo ya Bodi ya MWAUWASA kwenye mamlaka hizo, vilevile ilihusisha baadhi ya watumishi wa MWAUWASA kutoka vitengo mbalimbali ambao waliambatana na wajumbe wa Bodi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com