Frank Banati na Stella Kalinga,
Simiyu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliagiza
Shirika la viwanda vidogo nchini SIDO kuweka mikakati ya kupanua wigo wa
shughuli zake kwa kuanzisha vituo katika ngazi ya halmashauri za wilaya ili
kuwafikia wajasiliamali wengi zaidi, kuwajengea uwezo, kuwapa miongozo bora ya
namna ya kuendesha shughuli zao kwa tija na kuwaunganisha na taasisi za fedha
waweze kupata mikopo.
Waziri mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo
katika ufunguzi wa maonesho ya SIDO Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya
Nyakabindi Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu ambapo amesema umefika wakati kwa
SIDO kutilia mkazo sekta ya viwanda na hivyo kuifanya jukwaa la kuwakutanisha
wabunifu pia kuwapa fursa ya kuonyesha uwezo wao katika matumizi ya teknolojia
rafiki na rahisi zitakazoharakisha maendeleo ya viwanda nchini.
Pia
Waziri Mkuu Majaliwa amesema SIDO inapaswa kujielekeza katika kubuni mashine ,
mitambo na teknolojia rahisi zitakazotumika kuongeza thamani ya bidhaa na
kusisitiza kuwa kutokana na umuhimu wa sekta ya viwanda nchini katika
kukuza ajira na kuongeza pato la taifa serikali itaendelea kuweka miundombinu
wezeshi itakayoharakisha kasi ya ukuaji wa viwanda.
“
Bila shaka nyote mnafahamu tumedhamiria kufikia uchumi wa kati kufikia mwaka
2025, ninaamini tunao uwezo wa kulifikia lengo hili, sasa tunachotakiwa kufanya
kuhakikisha halmashauri zetu zote zinatenga maeneo maalumu kwa ajili shughuli
za viwanda kama mlivyofanya hapa Simiyu, lakini pia lazima mhakikishe
mnawajengea uwezo wajasiliamali ili waweze kuingia katika soko la ushindani,
alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa”.
Waziri
Mkuu Majaliwa amewasisitiza SIDO waendelee kubuni mikakati itakayoleta
mabadiliko katika sekta ya viwanda huku akiwataka wananchi kuthamini bidhaa
zinazotengenezwa hapa nchini ambazo tayari zimeonyesha kukidhi mahitaji ya
soko.
Halikadhalika
waziri Mkuu Majaliwa ameziagiza halmashauri za wilaya nchini kuendelea
kutekeleza agizo la kutenga 10% ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya
mikopo ya wanaweke, vijana na walemavu huku akiwasisitiza madiwani katika
halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa agizo hilo.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu Majaliwa ameupongeza uongozi wa mkoa wa Simiyu kwa
kujenga mahusiano mema na wananchi, viongozi wa kisiasa pamoja na taasisi
mbalimbali jambo ambalo amesema ni chachu ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi
na kijamii mkoani Simiyu.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda vidogo(SIDO), Prof.
Sylvester Mpanduji amesema Shirika hilo litaendelea kutoa mafunzo kwa
wajasriamali ili kuwajengea uwezo zaidi, ambapo amebainisha kuwa katika mwaka
wa fedha 2017/2018 SIDO imetoa mafunzo kwa wajasiriamali 16,900.
Aidha,
Prof. Mpanduji ameishukuru Serikali kwa kutenga shilingi bilioni 29 katika
mwaka wa fedha 2018/2019 ambazo zitasaidia kutatua changamoto mbalimbali za
wajasiriamali ikiwemo upatikanaji wa mashine mpya zitakazotumika katika vituo
vya SIDO vya kuendeleza viwanda, kukopesha wajasiriamali mitaji na kujenga
miuondombinu mingi ya viwanda katika sehemu hapa nchini.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amemhakikishia Waziri
mkuu kuwa Mkoa huo utahakikisha unaendelea kutekeleza maagizo ya
serikali ikiwemo agenda ya kitaifa ya Uchumi wa Viwanda kupitia Falsafa ya
Wilaya Moja Bidhaa Moja.
“Simiyu
ni Mkoa wenye ajenda na kazi yetu ni kutekeleza maelekezo na miongozo yote ya
Serikali, tunatekeleza Sera ya Viwanda chini ya Falsafa ya Wilaya Moja Bidhaa
Moja na sasa tunaenda kwenye utekelezaji wa Kijiji Kimoja Bidhaa Moja na sisi
tunaamini Mapinduzi ya Viwanda yanaanza na SIDO” alisema Mtaka.
Maonesho
hayo ya SIDO ambayo yanafanyika kwa mara ya kwanza mkoani Simiyu yamehudhuriwa
na wajasiliamali zaidi ya 500 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini ambayo
yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 28, 2018.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment