Zao la kahawa ni miongoni mwa mazao
matano ya biashara ambayo serikali ya awamu ya tano imeamua kwa dhati kutilia
mkazo uzalishaji wake, kwa mkoa wa Rukwa zao hilo ndio zao ambalo limeonekana
kustawi kwenye baadhi ya maeneo na kupelekea halmashauri za mkoa huu kutenga
shilingi milioni 79 kwaajili ya kununua mbegu ili kuendeleza zao hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo amesema kuwa kama mkoa hatuna budi kutilia mkazo uanzishaji na
uendelezaji wa zao hili ili wakulima wetu waweze kuwa na zao la biashara na
kubainisha kuwa tayari maeneo kwaajili ya kilimo hicho yameshabainishwa ambapo
makampuni, taasisi na wakulima wameonyesha nia ya kulima.
“Eneo la kiasi cha ekari 3,195.83 limebainishwa
kwa ajili ya kulimwa zao la kahawa. Jumla ya wakulima 2,266 na taasisi 9
zitajihusisha katika uzalishaji wa kahawa. zikiwemo taasisi za Jeshi la
Magereza pamoja na Jeshi la Wananchi Tanzania.”Alisema.
Ameyasema hayo katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa
(RCC) kilichofanyika mwezi huu wa nane katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa Mkoa
ikijumuisha wadau mbalimbali wa maendeleo, Wabunge, Madiwani, Viongozi wa dini
na wataalamu wa Halmashauri na sekretarieti ya mkoa.
Aidha, mbunge wa viti maalum Mkoa wa
Rukwa Mh. Aida Khenan amesema kuwa kilimo cha kahawa kinahitaji wakulima wenye
uwezo wa kifedha ambao katika mkoa wa rukwa wakulima hao hawapo na kusisitiza
kuwa wakulima wa mkoa huo wamezoea kilimo cha muda mfupi.
“kahawa inahitaji fedha na muda, wakulima
wetu wamezoea kilimo cha muda mfupi, watakaoweza kumudu kahawa ni wale wenye
uwezo, masuala ya madawa na kuhudumia hiyo kahawa, wataalamu wetu wafanye
utafiti watuambie zao lipi la kibiashara litaleta tija kwa wananchi wetu hasa
katika msimu huu wa kilimo,” Alisema.
Mh. Wangabo alieleza kuwa mkoa
umejipanga katika kuhamasisha kilimo cha zao la alizeti kama zao la kibiashara
kwani hali ya uzalishaji wa zao hilo kwa sasa hairidhishi na hivyo kutoleta
tija kwa wakulima.
“Hali ya
uzalishaji wa zao la alizeti katika Mkoa umebaki kuwa ni wastani
wa gunia 6.5 za kilo 65 kwa ekari sawa na tani 1.1 kwa
hekta. Tija hii ni ndogo sana ukilinganisha na tija iliyofanyiwa utafiti ya
gunia 12-16 kwa ekari ambazo ni sawa na zaidi ya tani 2.00 kwa hekta.” Alibainisha.
Serikali ya Awamu ya Tano imeamua
kutilia mkazo uzalishaji wenye tija wa mazao matano ya biashara ambayo ni
Korosho, Chai, Kahawa, Tumbaku na Pamba.
IMETOLEWA NA
OFISI YA MKUU WA
MKOA WA RUKWA
0 comments:
Post a Comment