Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Nkelei wilayani Lushoto ambapo pia alizindua huduma ya umeme katika Kijiji hicho.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (kushoto) akimkabidhi kifaa cha UMETA, Mbunge wa Bumbuli, January Makamba ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akiwasalimia wananchi katika Kijiji cha Mahezangulu katika Jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto mara baada ya kufika kijijini hapo kukagua kazi ya usambazaji umeme vijijini.
Afanya ziara wilayani Handeni,
Lushoto na kuwasha umeme katika Vijiji Vitano
Katika kuhakikisha kuwa adhma ya Serikali ya kusambaza
umeme katika vijiji vyote nchini ifikapo mwaka 2021 inatekelezwa, Waziri
wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amefanya ziara katika Wilaya ya
Handeni na Lushoto mkoani Tanga ili kukagua kazi za usambazaji umeme vijijini
na kuwasha umeme katika baadhi ya vijiji.
Akiwa wilayani Handeni, Waziri wa Nishati aliwasha umeme katika
Kijiji cha Madebe, Nyasa na Kwamnele na wilayani Lushoto aliwasha
umeme katika Kijiji cha Mabugai na Nkelei.
Aidha alifanya ziara katika kata na Vijiji mbalimbali ambavyo
bado havijasambaziwa umeme ikiwemo Kijiji cha Mahezangulu kilicho katika Jimbo
la Bumbuli, wilayani Lushoto ambapo aliagiza kuwa, kiwashiwe umeme ifikapo
tarehe 12 mwezi huu.
Katika ziara yake wilayani Handeni, Viongozi wa Wilaya hiyo
walimweleza kuwa, kuna vijiji 10 ambavyo vimepitiwa na miundombinu ya umeme
lakini havina nishati hiyo, hivyo kuleta malalamiko miongoni mwa wananchi kuwa
walitoa maeneo yao kupisha miundombinu hiyo lakini hawapati umeme.
Kuhusu suala hilo, Dkt Kalemani aliagiza kuwa, kuanzia Jumatatu
ya tarehe 8 Oktoba, 2018 wataalam wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) waanze
utaratibu wa kupeleka umeme katika Vijiji hivyo kwani kinachohitajika ni
kusambaza tu umeme kwa wananchi hao kwa kuwa miundombinu ipo.
Katika hatua nyingine, Dkt Kalemani alitoa onyo kuwa, Meneja
yeyote wa TANESCO atakayeonekana anatetea wakandarasi wanaochelewesha kazi kwa
kisingizio cha kutokuwa na vifaa atakuwa amejihesabia kuwa kashindwa kazi.
“ Hawa wakandarasi tayari wameshalipwa fedha za kuwawezesha
kuanza kazi ya usambazaji umeme vijijini, hivyo wanatakiwa kuwa na vifaa vyote
vinavyohitajika katika kazi hii,” alisema Dkt Kalemani.
Vilevile aliwataka watumishi kuwa na lugha ya staha pale
wanapohudumia wananchi na kueleza kuwa atakayeshindwa kufanya hivyo ataondolewa
katika nafasi yake.
Ziara ya Dkt Kalemani wilayani Handeni na Lushoto ilihudhuriwa
na viongozi mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Wilaya hizo, Wabunge, Madiwani na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January
Makamba.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment