Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko (kushoto) akizungumza na mmoja wa wanunuzi wa madini ya Kaolin, Andy He (kulia) kutoka kampuni ya Keda baada ya kutembelea machimbo/ migodi ya madini hayo katika wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.
Na George Binagi
Naibu Waziri
wa Madini Doto Biteko amefanya ziara ya kutembelea migodi ya madini ya Kaolini
katika wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani na kuwahimiza wawekezaji katika migodi
hiyo kuhakikisha wanalipa kodi stahiki za serikali.
Biteko
alifanya ziara hiyo jana na kukagua shughuli za uchimbaji madini katika migodi
ya RAK Kaolin Mining uliopo Kijiji cha Kimani pamoja na Abbeys katika Kijiji
cha Dalu na kusisitiza wawekezaji katika migodi hiyo kulipa kodi ya mrabaha
kutokana na bei ya kuuzia kiwandani na si bei ya mgodini.
“Sisi hiyo
tunaona ni kama utorokaji wa kodi na tumewasisitiza wachimbaji wetu wote wazingatie
sheria, walipe kwa kufuata bei wanayouzia kwenye kiwanda (Grose Value) na kwa
sehemu kubwa wamefanya hivyo kwenye migodi yote tuliyoitembelea”. Alisema
Biteko.
Aidha Biteko
alisisitiza kwamba sheria ya madini na kanuni zake za mwaka 2018, inasisitiza
kila mwenye leseni ya uchimbaji madini kutunza kumbukumbu za uzalishaji wake mgodini
na kwamba anayeshindwa kufanya hivyo adhabu yake ni faini kuanzia shilingi
Milioni 50 hadi 150 hivyo wenye migodi wahakikishe wanatunza taarifa zao muhimu
ikiwemo za uchimbaji na mauzo.
Katibu Tawala
wilayani Kisarawe, Mtela Mwampamba alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji
wilayani humo na kwamba serikali itaendelea kuwasimamia vyema kwa mujibu wa
sheria huku akibainisha kuwa changamoto za ulipaji fidia katika maeneo ya
wananchi zimetatuliwa kwa zaidi ya asilimia 90.
Mmoja wa
wawekezaji, Haji Nyambi ambaye ni Meneja Mgodi kutoka kampuni ya Abbeys Construction
inayochimba mchanga/ madini ya Kaolin katika Kijiji cha Dalu, aliomba
Halmashauri ya Kisarawe kujenga mizani ya kupima uzito wa magari ya kubeba
madini hayo tofauti na sasa ambapo wanalipa ushuru kwa kukadiria na hivyo bei
kubwa tofauti na mzigo halisi. Madini ya
Kaolin hutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali za ujenzi ikiwemo “Gypsum”.
0 comments:
Post a Comment