Waziri wa kilimo Tanzania-Mhe Dkt Charles Tizeba
Na Mathias Canal (WK), Dodoma
Kumalizika kwa Mkutano wa Mapinduzi ya
kijani Barani Afrika (AGRF 2018) mjini Kigali nchini Rwanda kumeongeza tija na
ufanisi kifikra kwa washiriki ikiwemo Tanzania kwa kuhakikisha kwamba wananchi
wanakuwa na mafanikio chanya kiuchumi kulingana na rasilimali zake nyingi za
asili ikiwemo ardhi yenye rutuba katika kilimo.
Afrika ina hekta milioni 600 za ardhi
isiyozalishwa ambayo ni sawa na asilimia 60 ya jumla ya kimataifa. Waziri wa
kilimo Tanzania-Mhe Dkt Charles Tizeba anaamini kwamba mafanikio katika kukuza
na kuimarisha uchumi Barani Afrika ni kupitia kilimo hivyo msisitizo mkubwa ni
kusimamia kiufasaha mikakati inayowekwa kwenye sekta hiyo kuliko mijadala
pekee.
Anasema Afrika inakadiriwa kuwa na idadi
kubwa kufikia bilioni mbili mwaka wa 2030 hivyo mapinduzi ya kilimo yanapaswa
kuimarisha mahusiano ya serikali na wananchi kwa kuwatunza wakulima kama wateja
na kuwapatia ujuzi na huduma bora ili kuongeza uzalishaji wa Mazao yao.
Kurejea kwa waziri wa kilimo Mhe Tizeba
leo tarehe 9 Septemba 2018 kunamfanya kuendelea na majukumu nchini mwake akiwa
na fikra chanya kupitia tukio la kila mwaka la kongamano la Mapinduzi ya kijani
(AGRF) linalowaweka pamoja wakuu wa nchi, wajasiriamali, wataalamu wa sekta na
wakulima kwa mazungumzo muhimu juu ya hali ya kilimo barani Afrika.
Waziri huyo wa kilimo nchini
Tanzania alipochangia mjadala kuhusu upotevu wa chakula baada ya uvunaji
alisema jambo hilo limeendelea kuwa tatizo kubwa siyo tu katika chakula lakini
pia katika malighafi kwa maendeleo ya viwanda huku akizitaja juhudi
zilizofanywa na serikali ya Tanzania kupunguza upotevu wa chakula.
Dkt Tizeba, alielezea juhudi
hizo kuwa ni pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, taasisi
za kimataifa kama vile Bill and Melinda Gates foundation, HELVETAS Swiss Inter
Cooperation Agency, Rockefeller foundation, AGRA, shirika la chakula Duniani,
mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yameboresha kwa kiasi kikubwa teknolojia
ya uhifadhi kama vile mifuko ya plastiki ya kuhifadhia nafaka ambayo imeonesha
kuwa na mafanikio makubwa sana kwa kuzuia wadudu waharibifu kupenya na
kushambulia nafaka.
Sambamba na hilo alisema juhudi
za kupambana na upotevu wa chakula kumeifanya Tanzania kuanzisha mfumo wa
kubadilishana bdhaa. Kuweka mazao katika masoko yaonekanayo ili kurahisisha
uuzaji na kupunguza upoteaji wa bidhaa za kilimo. Chini ya mradi huu mazao
yatatunzwa chini ya mfumo wa vikundi vya wakulima na kuuzwa moja kwa moja
katika mfumo wa kupitia soko la bidhaa.
Kongamano hilo limefika ukomo
hapo jana tarehe 8 Septemba 2018 baada ya kujadili maswala ya kilimo kwa siku
nne mfululizo, lilihudhuriwa pia na viongozi wengine wa Afrika akiwemo Rais wa
Ghana Mhe Nana Addo Dankwa Akufo Addo, Makamu wa Rais wa Kenya Mhe William
Ruto, Waziri Mkuu wa Gabon Mhe Emmanuel Issoze-Ngondet sambamba na Waziri Mkuu
mstaafu wa Uingereza Mhe Tony Blair.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment