Waziri wa Madini Angellah Kairuki (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wawekezaji kutoka Shirikisho la Madini ya Granite la nchini India na wataalam kutoka Wizara ya Madini na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Mwenyekiti wa Shirikisho la Madini ya Granite na Viwanda vya Mawe la nchini India, Keshava Murthy, akiweleza jambo Waziri wa Madini, Angellah Kairuki.
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati) akiongoza kikao kati ya Wawekezaji kutoka Shirikisho la Madini ya Granite la nchini India (Federation of Indian Granite & Stone Industry).
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amekutana Wawekezaji kutoka
Shirikisho la Madini ya Granite la nchini India (Federation of Indian Granite & Stone Industry) ambao
wameonesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta
ya Uongezaji Thamani Madini ya Mawe yenye thamani ya Granite na Mable.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika leo tarehe 18 Julai, jijini Dar
es Salaam, Waziri Kairuki ameueleza ujumbe huo kuhusu adhma ya Tanzania
kukakaribisha wawekezaji katika ujenzi wa vinu vya kuyeyusha madini ya metali, usonara pamoja na ukataji na ung’arishaji
madini ya vito hususan madini ya
Tanzanite ambayo kwa kiasi kikubwa yamekua yakisafirishwa nje ya nchi yakiwa
ghafi.
“ Sheria yetu ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya mwaka 2017,
imekataza usafirishaji wa Makinikia pamoja na madini ghafi nje, ndiyo maana
tunakaribisha wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye uongezaji thamani madini ndani ya nchi,” amesema Waziri Kairuki.
Pia, Waziri Kairuki amewashauri wawekezaji hao kukutana na Shirika la
Madini la Taifa (STAMICO) ili kuona namna bora ya kushirikiana katika miradi
mbalimbali ikiwemo ya mawe yenye thamani, bati na madini mengine.
Vilevile, Waziri Kairuki amelitaka shirikisho hilo kuona namna ambavyo linaweza
kushirikiana na wachimbaji wadogo wa madini nchini hususan katika masuala ya
masoko na mitaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Madini ya Granite na Sekta ya Mawe la nchini India, Keshava Murthy, amemweleza Waziri Kairuki kuwa, shirikisho
hilo liko tayari kuwekeza kwenye madini ya granite pamoja na marble kwa kuanza
na makontena kati ya 20-50 kwa mwezi.
Pia, Murthy ameongeza kuwa, Shirikisho hilo lina wanachama zaidi ya 1200
ambao wanajihusisha na shughuli za uongezaji thamani madini ya granite nchini
humo.
Kuhusu ushirikiano na STAMICO, Murthy amemwahidi Waziri Kairuki kuwa,
shirikisho hilo litakutana na shirika hilo kwa lengo la kubadilishana ujuzi
ikiwemo kuangalia namna bora ya kushirikiana katika sekta husika.
Aidha, amemweleza Waziri Kairuki kuhusu maonesho ya mawe yenye thamani yanayojulikana kama STONA FARE ambayo huandaliwa na
shirikisho hilo na kuongeza kuwa, ni
miongoni mwa maonesho makubwa duniani.
Mbali na kukutana na Waziri Kairuki, wawekezaji hao wanatarajia kuendelea
na ziara jijiji Dodoma ambapo wanatarajia kukutana na na Shirikisho la
Wachimbaji wa Madini Tanzania, kutembelea Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa
Madini Tanzania (GST) pamoja na kutembelea baadhi ya maeneo yenye uchimbaji wa
Granite jijini Dodoma.
Kabla ya kuja nchini, wawekezaji hao walitembelea nchi za Namibia,
Zimbabwe na Malawi kwa lengo la kutafuta fursa za uwekezaji kwenye madini hayo.
Kikao hicho pia, kimehudhuriwa na Mwakilishi kutoka Taasisi ya
Uwekezaji Tanzania (TIC), Wataalam kutoka Wizara ya Madini wakiongozwa na Kaimu
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Mashariki Mhandisi Ally Maganga
aliyemuwakilisha Kamishna wa Madini.
0 comments:
Post a Comment