METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, July 18, 2018

VIONGOZI WA KISIASA TUHAMASISHE WANANCHI KUENZI UTAMADUNI WAO - WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kuhitimisha  Sherehe za Mwakakogwa, eneo la Makunduchi Zanzibar Julai 18, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiingia kwenye eneo la Shereza za Mwakakogwa zilizofanyika Makunduchi, Zanzibar Julai 18, 2018. 
Sehemu ya umati wa watu waliohudhuria katika Sherehe za Mwakakogwa zilizofanyika  Makunduchi Zanzibar Julai 18, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishiriki katika sala ya kumwombea Rais wa Awamu ya Nne wa Zanzibar, Idris Abdul Wakil kwenye kaburi la Rais huyo enero la Makunduchi, Zanzibar Julai 18, 2018.  Wengine pichani kutoka kushoto ni Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Sira Ubwa  Mwamboya, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja , Ayoub Mohammed Mahmoud na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja,  Hassan Khatib Hassan. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akivalishwa kofia na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Sherehe za Mwakakogwa, Mwalimu Makungu Mwita katika sherehe za Mwakakogwa zilizofanyika Makunduchi Zanzibar Julai 18, 2018.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanasiasa wakiwemo mawaziri na wabunge wawahamishe Watanzania kuendeleza utamaduni wao.

Ametoa wito huo leo (Jumatano, Julai 18, 2018) wakati akizungumza na wazee na wananchi wa Makunduchi mara baada ya kushuhudia maadhimisho ya sikukuu ya Mwaka-Kogwa yaliyofanyika Makunduchi, wilaya ya Kusini, mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

“Mawaziri wote, tuna dhamana ya kuwahamasisha Watanzania waendeleze utamaduni ili uwe ni jambo hai. Wabunge na wawakilishi tukiwa kwenye majukwaa, tusisitize Watanzania waendeleze utamaduni,” amesema.

Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zinasimamia uwepo wa utamaduni na zenyewe zinaongozwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo imelenga kuihamasisha  jamii kuuenzi,  kuulinda na  kuudumisha utamaduni wa Mzanzibari na kushiriki katika uandaaji wa matamasha 50 ya utamaduni.

“Lazima utamaduni uendelezwe ndani na nje ya nchi na ni lazima tufanye jitihada tuwarithishe watoto utamaduni wetu. Kwa mfano, hapa Zanzibar mnalo tamasha la ZIFF, lile ni la kimataifa, vyombo vya muziki ni vya kisasa. Ni vema sasa, tukaangalia uwezekano wa kuwa na tamasha la huku chini ambalo litatumia ala za muziki za asili,” alisema.

Akizungumzia sherehe za Mwaka Kogwa, Waziri Mkuu alisema hii ni mara yake ya kwanza tangu azaliwe kuona watu wakichapana viboko si kwa ugomvi wala chuki, bali wakiwa na furaha.

“Mwaka Kogwa ni utamaduni wetu, pande zote za visiwani na zimekuwa zikifanyika kila mwaka lakini hivi sasa ni Makunduchi peke yake ambao mmeweza kuendeleza utamaduni huu, wengine wameacha kuadhimisha sherehe hizi,” amesema.

“Tanzania tuna makabila zaidi ya 120 wenye tamaduni na mila tofauti lakini si wote ambao wanaenzi mila na tamaduni zao. Utamaduni ni jambo muhimu nchini, utamaduni ni fursa ya kiuchumi kwa sababu watalii wanatoka kwao kuja Zanzibar kuangalia tukio kama hili, ni lazima tuuenzi,” alisisitiza.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewapongeza wakazi wa Makunduchi kwa kutunza na kuhifadhi mazingira na amewataka waendeleze bidii ya kuyatunza.

“Kati ya mambo ambayo nimeyapenda sana, ni tabia yenu ya uhifadhi mazingira. Lazima niwapongeze wana-Makunduchi kwa kutunza na kuhifadhi mazingira. Kama msingekuwa watu wazuri mgeshafyeka misitu yote, na kusingekuwa na mvuto kama nilivyoona. Endeleeni kuhifadhi mazingira yetu ili yaweze kututunza,” alisema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kusini, Bw. Hassan Khatib Hassan alisema wanafanya maadhimisho hayo ikiwa ni sehemu ya kuendeleza utamaduni na kuonyesha urithi kutoka kwa wazazi wao. “Tunaendeleza utamaduni huu sababu ni urithi kutoka kwa wazazi wetu. Ni upendo, amani na mshikamano,” alisema.

Mapema, Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Bw. Idrissa Kitwana Mustafa alisema wamewaalika mabalozi wa Uturuki na Iran kwenye maadhimisho hayo kwa sababu utamaduni huo pia unafanyika kwenye nchi zao.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi wa Makunduchi, Mwakilishi wa jimbo la Makunduchi, Bw. Haroun Ali Suleiman alisema anaipongeza serikali ya awamu y atano kwa mambo ambayo imeyafanya kwa kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

“Hakuna asiyeona, na kama mtu hataki kuona, basi hataona kabisa. TUnaomba utufikishie salamu zetu kwa Mhshimiwa Rais Magufuli,” alisema.

Alisema anaomba kuwe na ushirikiano wa karibu baina ya watendaji wa wilaya ya Kusini na ile ya Ruangwa ambako Waziri Mkuu anatoka ili watumishi wake waweze kubadilishana uzoefu na kuimarisha muungano.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com