MBUNGE wa Iramba Magharibi, Dk Mwigulu Nchemba ameahidi kutoa Sh milioni tatu na mifuko 500 ya saruji kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Kituo cha Afya katika tarafa ya Ndago, wilayani Iramba Mkoa wa Singida.
Akizungumza na wananchi wa eneo hilo jana wakati wa kukagua ujenzi huo, Dk Mwigulu alisema tarafa hiyo ilikuwa na zahanati ndogo ambayo ilikuwa haikidhi mahitaji wa wananchi wa eneo hilo.
Alisema kuwa wameamua kuongeza majengo ya wodi za kulaza wagonjwa, chumba cha upasuaji, chumba cha kuhifadhia maiti, wodi ya wakina mama, nyumba ya dakatari na maabara.
‘’Mwaka jana wakati nakabidhi gari la kubebea wagonjwa niliwaambia tutatengeneza kituo cha afya cha kisasa ili tuwe na Kituo chenye hadhi kama Hospitali ya Kiomboi. Katika kipindi hicho, tulipata Sh milioni 400 ndipo tukaanza ujenzi rasmi,’’ alisema Dk Mwigulu.
Alifafanua kuwa lengo la kuboresha zahanati hiyo ni kuwasaidia wananchi wasipate tabu ya kuwapeleka wagonjwa katika Hospitali ya Kiomboi ambayo ndio hospitali ya Wilaya hiyo.
‘’Tulitaka hospitali yenye hadhi ya hospitali ya wilaya licha ya kwamba maeneo mengine bado hatujamaliza lakini tutahakikisha kuwa tunamaliza na sasa ninatoa mifuko 500 ya saruji na ahadi ya Sh milioni tatu kwa ajili ya kukamilisha ujenzi,’’ aliongeza.
Pia alisema kuwa kwa wanataka kituo hicho kiwe na hadhi ya hospitali ya Wilaya, watahitaji wataalamu wenye hadhi hiyo kwa ajili ya kufanya upasuaji na wengine wa kutoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwajengea nyumba ya kuishi ili utoaji wa huduma upatikane wakati wote.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment