WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wasikubali kuchonganishwa na kwamba Serikali haiongozwi kwa misingi ya kidini bali imeziachia taasisi za kidini zifanye kazi kwa kuzingatia Katiba , Sheria za nchi na malengo yaliyokusudiwa katika uanzishwaji wake.
Aliyasema hayo jana jioni (Jumamosi, Juni 9, 2018) alipozungumza na viongozi na wananchi wa Mkoa wa Mwanza baada ya kushirikiana nao katika futari aliyowaandalia. Shughuli hiyo ilihudhuriwa na waumini wa dini mbalimbali.
Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wake wanaishi kwa amani na utulivu, jambo litakalowawezesha kufanya shughuli zao kikamilifu, hivyo wasikubali kuchonganishwa kwa misingi yoyote.
“Nawaasa viongozi wa dini msikubali kutumia makundi mengine nje ya taasisi zenu kwa ajili ya kuwazungumzia masuala yenu kwa sababu watawachonganisha na Serikali ambayo haipo kwa ajili ya kugombana na taasisi yoyote,” alisisitiza.
Waziri Mkuu alisema jukumu kubwa la taasisi za kidini ni kuhakikisha wanawalinda waumini wao pamoja na kuwaongoza kwa kuwapa mafundisho mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu, ambayo yatawawezesha kuishi kwa amani .
Alisema misingi ya amani na utulivu ikiwa pamoja na mshikamano walionao wananchi umesababisha Tanzania kupata heshima kubwa dunia kote, hivyo ni vema kila mwananchi ahakikishe suala la kudumisha amani linapewa kipaumbele.
Pia Waziri Mkuu alisema amefurahi sana kujumuika na wananchi wa Mkoa wa Mwanza katika futari hiyo, ambapo aliwapongeza kwa kukamilisha uundaji wa kamani za amani kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. John Mongella amlishukuru Waziri Mkuu kwa ukarimu wake kwa kuwaalika wakazi wa Mwanza katika hafla hiyo, ambapo alisema Mwanza ni kitovu cha amani kwa kanda ya Ziwa na nchi za Maziwa Makuu. T
“Mwanza tumejipanga na tunashirikiana na taasisi zote kwenye njanja zote , tupo pamoja na tunashirikiana katika kuimarisha amani na utulivu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli kwa kutuamini na tunamuahidi tutafuata falsafa zake katika utendaji wetu,”.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Mwanza na Askofu wa Kanisa la Charismatic Episcopal Church of Tanzania (CECT), Charles Sekelwa alisema wao wanaiunga mkono Serikali katika kudumisha amani na wataendelea kushirikiana nayo.
Alisema awali kulikuwa na changamoto ya matabaka ya kidini iliyobabisha na kutoelewana baina ya waislamu na wakiristo, ambapo kamati yao ilifanya kazi ya kuyasulisha na sasa hali ni shwari. “Matabaka ya kiimani yameisha na watu wa dini zote wanashirikiana vizuri,”.
Askofu Sekelwa alisema wao kama viongozi wa pande hizo mbili hawawezi kukubali kuona kunakuwa na matabaka ya kiimani miongoni mwa waumini, hivyo watakikisha wanaendelea kuwafundisha waumini wao umuhimu wa amani.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Naibu Spika Dkt. Tulia Akson, Naibu Waziri waNchi, OR – TAMISEMI, Joseph Kakunda, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali baadhi ya wananchi wa mkoa wa Mwanza
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JUNI 10, 2018.
0 comments:
Post a Comment