Mwenyekiti wa Jumuiya ya taasisi ya vyuo vya elimu ya juu
Tanzania (TAHLISO) akisoma tamko la Marais wa Vyuo vikuu katika mkutano
uliofanyika leo Chuo Kikuu cha Dodoma(Udom), Mjini Dodoma
Jumuiya ya Taasisi za
Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania(TAHLISO)imeyaonya wanaotumia kifo cha Mwanafunzi
Akwilina Akwilini kisiasa huku wakitumia mwamvuli wa jumuiya hiyo kutoa matamko
mbalimbali waache tabia hiyo vinginevyo watachukuliwa hatua.
Aidha, Jumuiya hiyo
imewaomba wanafunzi kuendelea kuwa watulivu kusubiri matokeo
ya uchunguzi wa kifo cha Akwilina na kujiepusha na maandamano na
vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani.
Onyo hilo limetolewa
leo mjini Dodoma na mwenyekiti wa jumuiya hiyo, George Mnali alipokuwa
akizungumza na vyombo vya habari wakati wa kikao na kamati tendaji ya Tahliso
kwa ajili ya kujadili changamoto zinazowakabili wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.
Kikao hicho
kimehusisha Marais wa serikali za wanafunzi wa Vyuo hivyo nchini.
Mnali amesema Tahliso
ndio chombo kikuu cha kuwasemea wanafunzi wote nchi nzima na sio kikundi
kingine chochote.
“Vipo vikundi vingi
vimejitokeza na kutoa matamko mbalimbali baada ya kifo hiki cha Mwanafunzi
mwenzetu Akwilina Akwilini kutokea, vikundi vingine vikaenda mbali zaidi kwa
kuwataka baadhi ya watendaji wa serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani
Kujiuzulu jambo ambalo linaashiria vikundi hivyo kutumika kisiasa,”amesema
Ameeleza kuwa
haiwezekani kutaka watendaji wa serikali wajiuzulu wakati uchunguzi bado
unafanyika na matokeo ya uchunguzi bado hayajatoka.
“Jambo la kusikitisha
zaidi kuna baadhi ya vikundi vimejitangaza kwamba vinaungwa mkono na Marais wa
Vyuo Vikuu jambo ambalo sio la kweli,”amesema Mwenyekiti huyo
Ametoa wito kwa
vikundi vyote vinavyojihusisha na kutumia mwamvuli wa Marais wa Vyuo Vikuu kama
kinga yao ilikuuhadaa umma kwamba wanaungwa mkono, viache tabia hiyo vinginevyo
watachukuliwa hatua.
Hata hivyo amesema Tahliso
wanasubiri matokeo ya uchunguzi unaofanyika juu ya kifo cha Akwilina na
wanatumai wahusika wote watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Amewaomba wanafunzi
waendelee kuwa watulivu wakati wanasubiri matokeo hayo nakujiepusha na
maandamano na vitendo vyovyote vinavyosababisha uvunjifu wa amani na kuleta
mgawanyo miongoni mwa wanafunzi.
Kadhalika, amesema
namna bora ya kufikisha hoja ni kutumia njia ya majadiliano kama wasomi badala
ya kutumia nguvu ya maandamano kwa kutofuata taratibu na madhara yake ni
kusababisha vurugu zisizotakiwa na hatimaye kuhatarisha usalama na hivyo
kuathiri jamii kwa ujumla wake.
Mnali amemshukuru Rais
John Magufuli kwa kuingilia kati suala hilo la kifo cha Akwilina na kuagiza
uchunguzi ufanyike na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wote watakaobainika
kuhusika na kifo hicho.
0 comments:
Post a Comment